TGNP Yapinga Uamuzi wa Bunge, Yataka Kamati ya POAC Irejeshwe

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Bi. Lilian Liundi

Na Mwandishi Wetu

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umepokea kwa masikitiko taarifa ya ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukusudia kuweka utaratibu wa kuzuia matangazo ya moja kwa moja kutoka Bungeni (Live) wakati vikao vya Bunge vinapoendelea, na badala yake vitarushwa baada ya kuhaririwa. TGNP pia imekerwa na uamuzi wa uongozi wa Bunge hilo kuifuta kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na TGNP kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao huo, Bi. Lilian Liundi imepinga kitendo cha Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah kutamka kuwa wanakusidia kupiga marufuku vikao vya Bunge kurushwa moja kwa moja kwa njia ya runinga.

Katika taarifa hiyo Bi. Liundi alisema wananchi wana haki ya kufuatilia mijadala inayowahusu, ikiwemo Vikao vya bajeti, miswada ya sheria na hoja mbalimbali za wananchi yakiwepo maswali ya wabunge kwa serikali juu ya kero na mahitaji ya wananchi bila kikwazo.
Aliongeza kuwa Serikali ya Tanzania imeridhia Tamko la Haki za Binadamu, Desemba 10, 1948 ambapo Kifungu cha 19 cha tamko (Article 19), kinachotoa uhuru wa mtu kutoa na kupokea mawazo bila kujali mipaka ya nchi na haki hii ya kutoa mawazo haipaswi kuingiliwa, hivyo kusudio la bunge linavunja tamko hilo.

“TGNP tumestushwa sana na Kitendo cha Spika wa Bunge, kuifuta Kamati ya POAC, ambayo imekuwa na ufanisi mkubwa katika kudhibiti mianya ya ufisadi katika sekta ya umma. Tunalaani kitendo cha kuifuta Kamati hii na sisi kama wanajamii tutaendelea kudai ulinzi wa rasilimali za Taifa hili na Bunge linapaswa kutuwakilisha ipasavyo katika kudai uwajibikaji wa watendaji wa serikali,” alisema Liundi katika taarifa hiyo.

Aidha aliongeza kuwa Tanzania ina jumla ya Mashirika ya Umma 258 yenye dhamani ya sh. Trilioni 10.2, hivyo kitendo cha kuifuta POAC kutatoa mwanya kwa mashirika haya kukosa usimamizi makini, jambo ambalo linaweza kusababisha wajanja kutumia mianya kufuja mali hizo za umma.

“Tunahitaji kamati ya Bunge makini ya kunusuru rasilimali hizi, la sivyo kwa vyovyote vile Taifa linarudi miaka ya kabla ya 2008, ambapo wizi wa EPA, MEREMETA, RICHMOND na ubinafsishaji holela wa mashirika ya umma ulifanyika,” aliongeza Bi. Liundi.

TGNP imelitaka Bunge kuhakikisha linaendelee kurushwa vikao vyake kama kawaida na wananchi wafuatilie kama ilivyokuwa hapo nyuma na Ofisi ya Bunge (kiti cha Spika) kuheshimu sheria, kanuni za kudumu za Bunge na haki ya wananchi ya kupata habari iliyoainishwa kwenye tamko la Haki za Binadamu Kifungu cha 19.

“Ofisi ya Bunge isiingilie mijadala ya wabunge na serikali hasa wabunge wanapodai uwajibikaji wa serikali kwa wananchi wake, ikiwa ni pamoja na wajibu wa serikali kutoa huduma za msingi za kijamii kwa wananchi kama maji, elimu, afya, miundombinu nk.”

“Tunamtaka Spika wa Bunge kufanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi ya nchi na historia ya uwajibikaji katika nchi. Waandishi wa habari waendelee kuwapiga picha wabunge wanaolala usingizi Bungeni ili wananchi waone aina ya viongozi wanaowapeleka Bungeni na kutokuwachagua tena kipindi kijacho.”
“…Kuzuia matangazo ya TV ni kukaribisha ufisadi, kuongeza utoro Bungeni na maovu mengine kufanyika kwa usiri kinyume na matakwa ya wananchi waliowatuma wabunge. Tunamtaka Spika wa Bunge kuirudisha mara moja Kamati ya POAC kabla ya Mkutano wa 11 wa Mwezi April 2013. Ofisi ya Bunge na Spika lazima zielewe kwamba Mamlaka yapo kwa wananchi na wao ni wasimamizi tu wa vikao vya Baraza la wananchi liitwalo Bunge. Wananchi ndio wenye mamlaka ya mwisho!”