CAF Yasitisha Ukamishna wa Hafidhi Ali, TFF Yazitakia Timu Mafanikio

Nembo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limesitisha ukamishna wa Hafidh Ali. Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika iliyokutana Januari 17 mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa CAF, Hicham El Amrani kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ukamishna huo umesitishwa kwa vile hadi sasa Shirikisho hilo halijapata ripoti ya mechi namba 78 kati ya Comoro na Libya ambayo Ali aliteuliwa kuisimamia.

Hivyo, ukamishna wa Ali umesitishwa hadi hapo CAF itakapopokea ripoti kuhusiana na mechi hiyo ambayo ilikuwa ni kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za AFCON zilizofanyika mwaka huu nchini Afrika Kusini.

KILA LA KHERI AZAM, JAMHURI, SIMBA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linazitakia kila la kheri timu za Azam, Jamhuri na Simba ambazo zinaiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Azam inacheza na Al Nasir Juba ya Sudan Kusini katika mchezo wa Kombe la Shirikisho utakaofanyika Jumamosi (Februari 16 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Nayo Jamhuri ya Zanzibar kesho itacheza na St. Georges ya Ethiopia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaofanyika Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba. Simba itacheza na Recreativo do Libolo ya Angola keshokutwa (Februari 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

YANGA, AFRICAN LYON ZAINGIZA MIL 68/-

Mechi namba 119 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa juzi (Februari 13 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Yanga kuibuka ushindi wa mabao 4-0 imeingiza sh. 68,438,000.

Watazamaji 12,147 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 16,170,252.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 10,439,694.92.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo 10,982 walikata tiketi hizo na kuingiza sh. 54,910,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 8,222,162.26, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 4,933,297.36, Kamati ya Ligi sh. 4,933,297.36, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,466,648.68 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,918,504.53.

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA TASMA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Februari 10 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TASMA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia tiba ya wanasoka nchini.

TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TASMA chini ya uenyekiti wa Dk. Mwanandi Mwankemwa aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo kwa kura 18 dhidi ya 7 za aliyekuwa Mwenyekiti Biyondho Ngome

Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba ya TASMA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.

Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA chini ya Dk. Paul Marealle na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Safu nzima ya uongozi wa TASMA iliyochaguliwa inaundwa na Dk. Mwanandi Mwankemwa (Mwenyekiti), Dk. Nassoro Matuzya (Katibu Mkuu), Sheky Mngazija (Katibu Msaidizi), Dk. Juma Mzimbiri (Mhazini), Joakim Mshanga (mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF) na Dk. Hemed Mziray (mjumbe wa Kamati ya Utendaji).

Ukiondoa nafasi ya Mwenyekiti, wagombea wengine wote hawakuwa na wapinzani. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti haikupata mgombea, hivyo itajazwa katika uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye mwaka huu.