Na Mwandishi Wetu, Mara
WAKATI watu mbalimbali wakisherehekea siku ya wapenda nao (Valentine Day), Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Japhet Lusingu anasema wanawake watatu wameuwawa baada ya kupigwa na waume zao katika matukio tofauti. Kuuwawa kwa wanawake hao kunatimiza idadi sita ya matukio ya vifo mkoani Mara, huku wengine tisa wakijeruhiwa.
Akizungumza na wanahabari jana mjini hapa, Lusingu alisema matukio hayo yametokea kati ya mwezi Januari na Februari mwaka 2013.
Akifafanua matukio hayo Lusingu alisema tukio la kwanza lilitokea Februari 10, 2013 majira ya saa 3:00 asubuhi Kijiji cha Tonyo Kata ya Busumwa, Wilaya ya Butiama,ambapo mwanamke aliyetambulika kwa jina la Happyness Lucas (25), alipigwa na mumewake, Rugera John (27) hadi kusababisha kifo chake.
Alisema chanzo cha ugomvi huo ni ndala (kandambili) ambazo mume wa marehemu alikuwa amemnunulia mke mdogo. Happyness Lucas ambaye kwa sasa ni marehemu alipelekwa katika Hospitali ya Butiama kwa matibabu baada ya kipigo lakini Februari 11 alifariki dunia.
Kaimu Kamanda Lusingu alisema tukio jingine lilitokea Januari 28, 2013 wilayani Bunda, Mtaa wa Chiringe, ambapo Rhobi Lucas (24) fundi cherehani akiwa nyumbani kwake alifika mumewe aliyetajwa kwa jina la Masumbuko Khamis akiwa na hawara yake, Joyce Manumbu.
Inadaiwa kuwa baada ya kufika mume wake alianzisha ugomvi na kuanza kumshambulia mke wake kwa mateke huku akishirikiana na hawara yake. Baada ya ugomvi Rhobi Lucas aliamua kuondoka nyumbani kwake na kwenda kwa wazazi wake kutoa taarifa za kushambuliwa siku hiyo hiyo.
Aidha Kamanda Lusingu aliongeza kuwa Januari 30, 2013 mumewe pia (Masumbuko) alifika Polisi kutoa taarifa kuwa ameshambuliwa na mkewe baada ya taarifa hiyo mkewe alikamatwa na Januari 31 alifikishwa mahakamani.
Aliongeza kuwa Februari 9, 2013 mwanamke huyo alizidiwa na hali yake kuwa mbaya kutokana na kipigo alichokipata toka kwa mumewe kwa kushirikiana na hawara yake na kupelekwa Hospitali ya DDH Bunda kwa matibabu, lakini Februari 11 alifariki dunia. Polisi wanamshikilia mwanaume huyo kuhusiana na kifo hicho.
Tukio lingine lilitokea Februari 9, 2013 saa 9:00 jioni Kijiji cha Nambubi Tarafa ya Nansimo wilayani Bunda, ambapo mwanamke aliyejulikana kwa jina la Edith Christopher (36) alishambuliwa na mumewe Elephasi Maitabo (58) na mpini wa mundu kwa kupigwa tumboni, mgongoni na kifuani na kufariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali.
Chanzo cha mauaji hakijajulikana lakini mtuhumiwa huyo amekamatwa na polisi na atafikishwa mahakamani mara taratibu zitakapokamilika.
Tukio la tatu, lilitokea Februari 11, mwaka huu saa 1:30 asubuhi maeneo ya Kijiji cha Mkirira wilaya ya Butiama, ambapo mwanamke aliyejulikana kwa jina la Ziada Sasita (35) mkazi wa Kijiji cha Kabegi aliuawa kwa kunyongwa shingo kwa kutumia nguo yake (mtandio) hadi kufa na watu wasiojulikana.
Marehemu alikuwa anatokea kwa mjomba yake maeneo ya Mkirira ambako alikwenda kumsalimu na mauti yalimkuta akirejea Kabegi ambako alikuwa ameolewa. Mwili wa marehemu ulikutwa na mtandio shingoni na ulimi wake ukiwa umetoka nje. Hadi sasa hakuna anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo.
Tukio lingine ni ajali ya mwendesha pikipiki kugonga kizuizi cha standi mpya ya mabasi wilayani Bunda ambapo mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Maka umri kati ya miaka 18 hadi 20 akiwa na pikipiki isio na namba za usajili, chanzo cha ajali ni mwendo kasi.
Tukio la lingine lilitokea Februari 10 mwaka huu saa 4:15 usiku Kijiji cha Msinganyi, Bunda ambapo gari aina ya Fuso namba T 677 BLQ mali ya Masunga Bugubugu mkazi wa Bariadi iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ambaye hajafahamika jina lake hadi sasa.
Gari hiyo ilikuwa inatokea Kijiji cha Kenyamonta Wilaya ya Serengeti mnadani iliacha njia na kupinduka na kusababisha kifo cha Magoti umri kati ya miaka 35 hadi 40, mfanyabiashara wa wilaya ya Butiama na wengine tisa kujeruhiwa.
Kamanda Lusingu aliwataja waliojeruhiwa ni Grace Masoka (40), Prisca Gwasi (42), Chausiku Mashara (35), Neema Hamis (25), Chacha Mwita (34), jamwela Wambura (30), Hassan Bunge (34), Juma Komba (22) na mary Rashid (37) wote wakazi wa Wilayani Bunda.
Kamanda Lusingu ametoa wito kwa wanaume wa Mkoa wa Mara kuacha kutumia nguvu na mabavu kwa wake zao kwani matukio ya aina hiyo yamezidi.
Chanzo Binda News