CAG Kufanya Kazi za Ukaguzi kwa Mtandao

Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh akipokea cheti cha kukamilika kwa mradi wa kuiunganisha ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka kwa Bw. Kisamba Tambwe (kulia) Meneja wa njia za Mawasiliano za nje kutoka Kampuni ya simu Tanzania (Picha zote na Aron Msigwa-Maelezo).

Na Aron Msigwa – MAELEZO

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) imeingia katika mfumo mpya wa mawasiliano wa matumizi ya barua pepe na intaneti utakaoiwezesha ofisi hiyo kutuma na kupokea taarifa za utendaji kwa haraka kufuatia kukamilika kwa mradi wa kuunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam wakati wa makabidhiano ya mradi huo uliofanywa na kampuni ya Simu Tanzania, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh amesema kuwa mradi huo utaiwezesha ofisi yake kuimarisha mawasiliano ya ndani na nje ya ofisi kupitia mfumo wa intaneti.

Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh (katikati mbele) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Ofisi hiyo na viongozi wa Kampuni ya Simu Tanzania TTCL leo jijini Dar Es salaam.


Amesema mradi huo ambao kwa sasa umeanza kwa kuziunganisha ofisi 12 za mikoa mbalimbali utaleta mabadiliko makubwa katika nyanja nzima ya upashanaji habari na utawawezesha watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za serikali kupata mawasiliano kwa kwa haraka na usalama zaidi kupitia makao makuu ya ofisi hiyo.

Amesema mkongo wa taifa utaiwezesha ofisi hiyo kumiliki na kudhibiti taarifa mbalimbali zinazotumwa kwa kuwatumia wataalam wa Tehama wa ndani huku akibainisha kuwa mfumo huo mpya utawazuia watumishi wa ofisi hiyo kutumia mifumo ya kawaida ya barua pepe na mitandao hatarishi inayoweza kuleta madhara kwenye taarifa muhimu za serkali.

“Mradi huu umekamilika wakati muafaka kwa sababu utatuwezesha kupunguza gharama, kumiliki na kudhibiti sisi wenyewe taarifa zetu za kiutendaji za kila siku kupitia wataalam wa Tehama tulionao katika ofisi zetu na kuondoa kabisa mfumo uliokuwepo wa kubeba taarifa mikononi kutoka eneo moja hadi jingine” amesema Utouh.

Amefafanua kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali nchini kujenga uwezo wa uimarishaji wa miundombinu za shughuli za Ukaguzi na utendaji na kurahisisha mawasiliano kwa kutumia mfumo wa kompyuta huku akifafanua kuwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali Tanzania kwa kipindi cha miaka 6 ni wakaguzi wa Umoja wa mataifa ukaguzi unaofanywa katika miji mbalimbali duniani.

Utouh amebainisha kuwa ofisi yake sasa itaweza kufanya mikutano ya kiutawala moja kwa moja na ofisi za mikoani kupitia mfumo mpya wa mawasiliano wa mtandao (video conference) na kuwataka watumishi wa ofisi hiyo kuutumia ipasavyo mfumo huo kwa manufaa ya taifa.

Kwa upande wake Meneja wa njia za mawasiliano ya nje wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Kisamba Tambwe akikabidhi mradi huo amesema kuwa kampuni hiyo imetekeleza mradi huo kwa ufanisi mkubwa ili uweze kukidhi malengo yaliyokusudiwa.

Amesema TTCL itaendelea kuhakikisha kuwa ofisi 12 za mikoa iliyouganishwa kwenye Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa zinakuwa na usambazaji salama wa taarifa kutoka eneo moja hadi jingine.