SMZ Kupambana na Wanaodhalilisha Watoto

Wanafunzi wa madrasatul Maamur ya Tumbatu Jongowe
wakisoma Qaswida wakati wa maulid ya Mtume Muhammad (SAW) yaliyofanyika jana katika zawia ya kijijini hapo. [Picha na Ramadhan Othman Ikulu]

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein akikata utepe kufungua zawia ya Tumbatu Jongowe alipohudhuria katika maulidi ya Mtume Muhamad (SAW) yanayosomwa kila mwaka katika kijijini hapo.[Picha na Ramadhan Othman Ikulu]



Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein amewataka waumuni wa dini ya Kiislamu kufuata maadili na mwenendo wa Mtume Mohammad (S.A.W) na kuwafunza watoto maadili hayo huku akiisitiza kuwa Serikali haitowafumbia macho wale wote wanaowadhalilisha watoto wadogo.

Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo katika sherehe za Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Mohammad (S. A. W) yaliyofanyika huko Tumbatu Jongoe, Mkoa wa Kaskazini Unguja. Katika maelezo yake Alhaj Dk. Shein alieleza haja ya kumfanya Bwana Mtume Mohammad S.A.W kuwa kigezo kwa Waumini wa Kiislamu kutokana nay eye kuwa na maadili mema.

Alisema kuwa kutokana na hatua hiyo kuna kila sababu kwa wazee nao kuwafundisha maadili mema watoto wao na kusema kuwa Serikali imelifalia njunga suala la kuwadhalilisha watoto ikiwa pamoja na kuwabaka.

Baadhi ya Akina Mama wa Tumbatu Jongowe na Vijiji Jirani walioalikwa katika maulidi ya Mtume Muhammad (SAW) wakiwa nje ya zawia ya kijijini hapo palipofanyika Maulid hayo. [Picha na Ramadhan
Othman Ikulu]


Alieleza kuwa kutokana na hali hiyo ndio maana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetunga Sheria maalum katika juhudi za kuwalinda na kuwatunza watoto ili kuepuka kadhaa ya kuwadhalilisha watoto wadogo.

Alhaj Dk. Shein alisema kuwa jambo hilo limepigwa vita hata katika dini ya Kiislamu na kusisitiza kuwa mara zote uislamu unasisitiza kuwaenzi, kuwafuza, kuwatunza na kuwafundisha maadili mema watoto huku akiwapongeza wazee wa Tumbatu Jongoe kwa kuwapa maadili mema watoto wao.

Alisema kuwa wazee wa Tumbatu Jongoe wamechukua hatua kubwa katika kuwapa maadili mema watoto hao na ushahidi umejionyesha katika sherehe hizo kutokana na watoto hao kuonesha mafuzo mema waliyoyapata kutoka kwa wazee na waalimu wao.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja kwa Waislamu kusoma elimu ya dunia na akhera ili waweze kuishi maisha bora zaidi zaidi. Katika hotuba yake hiyo, pia, Dk. Shein aliwasisitiza wazee wa Tumbatu Jongoe nao kuendelea kusoma na kutafuta elimu kwani elimu haina mwisho.

Alisema kuwa jambo kubwa katika maisha ya binaadamu ni kusoma hivyomalisisitiza wazee hao kuwafunza watoto pamoja na wao wenyewe kujifunza Qur-an kwani maisha ya dunia ni ya kupita. “Malezi mnayowapa watoto wetu hawa yamenipamoyo mkubwa”,alisisitiza Dk. Shein.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa dini ya Kiislamu ni dini ya amani na upendo hivyo aliwataka waumini hao kuendelea kuishi kwa amani na utulivu kama dini hiyo inavyosisitiza.

Alhaj Dk. Shein aliwaeleza waumini hao wa Tumbatu Jongoe kuwaepuka wale wote wanaodhamiria kuleta shari huku akisistiza kuwa Serikalimara zote imekuwa ikihubiri amani, umoja na mshikamano.

Katika shehehe hizo Alhaj Dk. Shein alianza kwa kufungua jengo hilo jipya la Zawia la Kijiji hicho ambalo litatumika katika kufanyia shughuli kama hizo za kidini pamoja na shughuli nyengine za kijamii.

Alhaj, Dk. Shein alitoa pongezi kwa wale wote waliotoa rai ya ujenzi huo pamoja na waliochangia ujenzi huo. Pia, alitoa pongezi kwa mapokezi aliyofanyiwa.

Mapema Dk. Shein alifanya mazungumzo na wazee wa Tumbatu Jongoe na kuwahakikishia kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wake na wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni pamoja na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili.

Nao wananchi, wazee, na Tumbatu Jongoe walimpongeza Alhaj Dk. Shein kwa kuungana nao katika shrehere hizo kubwa za kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambazo hufanyika kila mwaka kijijini kwao hapo.

Walieleza kuwa Dk. Shein ameoesha imani kubwa kwa wananchi wa kijiji hicho kwa kuwakubalia ombi lao hilo, ambapombali ya sherehe hizo wazee wa kijiji hicho walimpa zawadi mbali mbali Alhaj Dk. Shein ambaye nae alitoa shukurani kuwa kwa zawadi hizo kikiwemo cheti maalum walichomtunuku kutokana na mapenzi yao makubwa kwa kiongozi huyo.