RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amekwenda Mozambique leo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambako atahudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mkutano huo uliopangwa kufanyika baadaye leo, utakuwa chini ya uenyekiti wa Rais Emilio Armando Guebuza, Rais wa Mozambique ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa SADC. Kikao hicho kitajadili maendeleo katika juhudi za SADC kutafuta ufumbuzi wa migogoro ambayo Jumuia hiyo imekuwa inaishughulikia karibuni na inayohusu nchi wanachama wa Jumuia hiyo – yaani hali ya kisiasa katika Madagascar na Zimbabwe na hali ya kiusalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako majeshi ya waasi wa M23 yanakabiliana na majeshi ya Serikali ya Rais Joseph Kabila.
Wakati huo huo; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kuomboleza kifo cha Askofu mstaafu Amedeus Msarikie wa Jimbo la Moshi.
Askofu Msarikie aliaga dunia Alhamisi, Februari 7,2013 katika hospitali moja ya mjini Nairobi, Kenya ambako alikuwa anatibiwa akiwa na umri wa miaka 82.
Rais Kikwete katika salamu zake za rambirambi kwa Rais huyo wa TEC amesema: “Nimehuzunishwa na kusikitishwa na taarifa za kifo cha Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie ambaye nimejulishwa kuwa aliaga dunia jana mjini Nairobi, Kenya ambako alikuwa anapata matibabu hospitalini.”
Amesema Rais Kikwete: “Askofu Msarikie ambaye alistaafu rasmi mwaka 2007 baada ya kuliongoza Jimbo la Moshi kwa miaka 22, atakumbukwa kwa mengi. Alikuwa kiongozi hodari wa kiroho. Alikuwa pia mwalimu mwenye sifa za kutukuka. Askofu alitoa mchango mkubwa katika elimu na mchango wake katika maendeleo ya sekta hiyo hautasahahulika kamwe. Alikuwa mkereketwa wa elimu na alichangia sana kuinua kiwango cha elimu katika Mkoa wa Kilimanjaro.”
“Kwa niaba ya serikali ninayoiongoza na kwa niaba yangu mwenyewe, nakutumia wewe Baba Askofu Ngalalekumtwa salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo cha Baba Askofu Msarikie. Aidha, nakusihi upokee salamu zangu za pole nyingi kwa viongozi wote na waumini wa Kanisa Katoliki katika Jimbo la Moshi na Tanzania nzima kwa kuondokewa na kiongozi wao, askofu wao na mwalimu wao,” amesema Rais Kikwete na kumalizia:
“Baba Askofu Ngalalekumtwa, naungana nawe, viongozi wenzake na waumini wote wa Kanisa Katoliki Tanzania kuomboleza msiba huu mkubwa. Msiba huu ni wetu sote na machungu ni yetu sote. Aidha, naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema poponi roho ya Marehemu Askofu Amedeus Msarikie. Amen.”