ALIYEKUWA Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk. Thomas Laizer aliyefariki juzi mkoani Arusha anatarajiwa kuzikwa Ijumaa kanisani. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Askofu Mkuu wa KKKT Tanzania, Dk Alex Malasusa leo jijini Dar es Salaam marehemu askofu Laizer atazikwa ndani ya kanisa lake alilokuwa akiliongoza.
Dk Malasusa alisema waumini na wananchi, ndugu jamaa na marafiki watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho kwa Mwili wa marehemu Thomas Laizer kuanzia siku ya Alhamisi ya Februari 14, 2013 kabla ya mazishi kufanyika Siku ya Ijumaa. Wakati huo huo familia ya marehemu askofu Laizer imewataka Watanzania kumuombea kiongozi huyo wa kiroho kwa Mungu.
Akizungumza mjini Arusha nyumbani kwa marehemu askofu Laizer mmoja wa watoto wake alisema njia hiyo ndiyo sahihi katika kipindi hiki kigumu cha msiba wa baba yao, aliongeza kuwa hakuna binadamu asiyekuwa na mapungufu hivyo kuwaomba wamsamehe kama lilitofautiana nao.
Marehemu askofu Laizer aliyezaliwa Machi 10, 1945 katika Kijiji cha Kitumbeni mkoani Arusha na baade kupata elimu yake ya msingi Longido (mwaka 1965), alifariki kwa ugonjwa wa saratani akipata matibabu hospitalini. Askofu Thomas Laizer ameacha mjane na watoto wanne na mjukuu mmoja.