MAHAKAMA inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imebatilisha uamuzi wa kesi iliyowahusu mawaziri wawili wa zamani nchini Rwanda na kuamuru waachiliwe mara moja. Justin Mugenzi na Prosper Mugiraneza walihukumiwa miaka 30 jela mnamo mwaka 2011, kwa kuhusika na mauaji hayo pamoja na uchochezi wa watu kufanya mauaji.
Wadadisi wa mambo wanasema Serikali ya Rwanda huenda ikaghadhabishwa na hatua ya kuachiliwa kwa wawili hao. Takriban watu 800,000, wengi wao wa kabila la Tutsi pamoja na waHutu waliuawa mwaka 1994, katika mauaji hayo ya kimbari.
Bwana Mugenzi alikuwa waziri wa biashara wakati wa mauaji hayo wakati bwana Mugiraneza alikuwa waziri aliyehusika na maswala ya wafanyakazi wa umma. Mahakama maalum iliyoundwa kwa ajili ya mauaji ya Kimbari Rwanda, (ICTR), iliwapata na hatia ya kuhudhuria mkutano ambao uliamua kufurushwa kwa kiongozi wa eneo la Butare Kusini mwa Rwanda, kwa kuzuia mauaji kufanyika.
Pia walipatikana na hatia ya kuhudhuria mkutano wa kaimu rais Theodore Sindikubwabo aliyewasihi watu kuwaua waTutsis. Jaji wa mahakama ya rufaa, aligundua kuwa bwana Mugenzi na mwenzake Mugiraneza hawakujua kuwa nia ya Sindikubwabo ilikuwa ni kutoa hotuba.
Majaji pia walisema kufurushwa kwa kiongozi wa Butare, Jean-Baptiste Habyarimana, huenda ulikuwa uamuzi wa kisiasa na wala sio kuharakisha mauaji ya kimbare.
Aidha wadadisi wamesema kuwa serikali huenda ikakasirishwa sana hasa kwa kuachiliwa kwa bwana Mugiraneza ambaye alikuwa mtu mashuhuri serikalini na aliyehusika pakubwa na mauaji ya kimbari.
Serikali ya Rwanda inayoongozwa na waliokuwa waasi wa KiTutsi na ambao walipigana dhidi ya serikali iliyosababisha mauaji ya Kimbari, imekuwa ikikashifu vikali mahakama ya ICTR, na kusema inajikokota pamoja na kugharimu pesa nyingi. Lakini ICTR imekuwa ikijitetea ikisema kuwa kesi za Genocide katika mahakama za kimataifa huwa zina changamoto zake.
Mahakama ya ICTR inatarajiwa kufungwa mwaka 2014 baada ya kusikiliza kesi zingine 15 za rufaa. Kulingana na mahakama hiyo, imesikiliza kesi 70 tangu kufunguliwa kwake kuambatana na azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa Novemba mwaka 1994 hususan kusikiliza kesi za washukiwa wakuu wa mauaji hayo.
-BBC