Raia Mwema lashinda dhidi ya FCC

Gazeti la Raia Mwema

Baraza la Habari Tanzania (MCT) jana lilisikiliza mashauri mawili yanayohusiana na vyombo vya habari kukiuka maadili ya uandishi na kuyatolea maamuzi.

Shauri la kwanza lilihusu Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), kupitia gazeti lake la The Citizen ambalo lilidaiwa kuandika habari zilizokuwa sahihi zilizodai kwamba Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimekumbwa na kashfa ya ufisadi kwa mujibu wa ripoti ya hesabu za kati ya mwaka 2006 na 2012.

Kamati ya Maadili chini ya Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo, baada ya kupitia hoja za pande zote za mlalamikaji na mlalamikiwa, lilitoa maamuzi ya kuwakutanisha tena ndani ya siku 14 ili kuangalia hali ilivyo sasa.

Jaji Mihayo alisema sekretarieti ya MCT itaratibu mkutano mwingine na kwamba matokeo yatakayopatikana yachapishwe katika gazeti la Citizen ndani ya siku saba.

Kwa upande mwingine, Tume ya Ushindani (FCC) jana iliwasilisha kwa MCT malalamiko yake dhidi ya gazeti la Raia Mwema ikiomba habari iliyoandikiwa dhidi yao ikanushwe.

Baada ya kutolewa hoja za pande mbili, MCT chini ya Jaji Mihayo ilipitisha maamuzi kwamba kutokana na nyaraka zilizowasilishwa na gazeti hilo halikuona makosa yoyote yaliyojitokeza.

Jaji Mihayo alisema Raia Mwema halina kosa kutokana na kuandika habari zilizohusisha FCC na kujihusisha na vitendo vya rushwa na kusema kamati ya maadili ya MCT imeridhika na ushahidi wa mlalamikiwa.

CHANZO: NIPASHE