Na dev.kisakuzi.com
VYOMBO vya habari nchi vimeombwa kutoa elimu kwa jamii
juu ya manufaa ya iwepo wa Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano (National ICT Broadband Backbone-NICTBB)
ili wananchi wauelewe na kuulinda kutokana na umuhimu
wake.
Changamoto hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na
Meneja Uendeshaji wa NICTBB, Adin Mgendi alipokuwa
akizungumza na wahariri wa vyombo anuai vya habari juu
ya utendaji kazi wa mkongo huo na manufaa yake kwa
taifa.
Mgendi alisema manufaa ya ujenzi wa Mkongo wa
mawasiliano nchini yameanza kujitokeza hivyo
Watanzania wana kila sababu ya kuulinda mtandao huo
kwani unaumuhi mkubwa kwa jamii na taifa.
Alisema kwa sasa jumla ya nchi sita, ambazo ni pamoja
na Malawi, Zambia, Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya
zimeunganishwa na Tanzania hivyo nchi yetu ikibeba
dhamana ya kuwahudumia kupitia mtandao wa Mkongo.
Mtalamu huyo alivitaka vyombo vya habari kuendelea
kutoa elimu kwa wananchi hasa waliopo karibu na njia
ya mkongo ili wasiuharibu kupitia shughuli mbalimbali
za kijamii zinazofanyika ardhini.
Akifafanua zaidi kwa wahariri wao, Ofisa Biashara wa
Mkongo, Thomas Lemunge alisema kwa sasa mikoa yote ya
Tanzania Bara tayari imeunganishwa na mkongo hivyo
kurahisisha miundobinu ya mawasiliano.
Aidha aliongeza kuwa mtandao wa mkongo ambao ujenzi
wake uaendelea umepita maeneo anuai; ikiwemo ardhini
pembezoni mwa barabara, mashambani, juu ya nyaya za
umeme na kwenye maji huku ukiwa na mizunguko mitatu
yaani wa Kaskazini, Magharibi na Kusini.
Awali akizungumza na washiriki hao, kabla ya kufungua
warsha hiyo, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano nchini (TEHAMA), Mhandisi Zaipuna Yonah
alisema mkongo unamanufaa makubwa kwani hadi sasa
matumizi ya intaneti yameongezeka tofauti na awali.
“Ongezeko la matumizi na faida za mkongo zinaongezeka
siku hadi siku na hivyo kukidhi matarajio ya Serikali
ya kuziba pengo la matumizi ya TEHAMA kwa wananchi
katika maeneo ya mbalimbali ya nchi yetu na hatimaye
kukuza uchumi,” alisema Yonah.
Wahariri hao walipata fursa ya kutembelea kituo kikuu
kinachoratibu shughuli za mkongo maeneo mbalimbali ya
nchi na kuona namna wataalamu wanavyofanya kazi eneo
hilo.
Mkongo wa taifa ambao kwa sasa unategemewa na nchi
jirani za Tanzania na makampuni binafsi katika
usabazaji huduma za mawasiliano unasimamiwa na Kampuni
ya Simu Tanzania (TTCL) huku wakiwa ndio meneja wa
Mkongo huo.