MFUKO wa Bima ya Afya (NHIF) umetoa msaada wa mashuka 200 yenye dhamani ya shilling 3,000,000 kwa ajiri ya hospitali ya Rufaa ya Bombo ya Mkoa wa Tanga leo tarehe 30/01/2013. Msaada huo umetolewa kwa ajiri ya kukabiliana na tatizo la uhaba wa mashuka uliopo kwa sasa.
Akizungumza wakati wa kukabithi mashuka hayo kwa Mkuu wa Mkoa Mh. Chiku Gallawa hospitalini hapo, Meneja wa Mfuko huo Ndg Ally Mwakababu amesema NHIF itaendelea kusaidia Hospitali ya Bombo na vituo mbalimbali vya kutolea huduma ili kuboresha huduma za afya .
“Mfuko umekuwa na jitihada mbalimbali katika kuhakikisha huduma za afya vituoni zinakuwa bora na unafanya hivyo kwa kutambua kuwa afya ndio muhimili mkubwa wa mtanzania katika kufanya kazi na kujiondolea umasikini “
Akikabithi msaada huo kwa Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Dr Ally Uredi, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wauguzi na madaktari kuwa na moyo wa uzalendo katika kutunza vifaa vya huduma za afya ili kuleta chachu ya maendeleo katika sekta hii nyeti.
Pia ametoa wito kwa wananchi kutambua kuwa Hospitali ya Bombo ni kwa ajiri ya wagonjwa wa Rufaa tu. Imewapasa Wananchi kuwa na mazoea ya kutibiwa katika vituo vya afya vilivyoko wilayani mwao. Hii itaipatia fursa hospitali ya Bombo katika kutekeleza jukumu lake la kuuhudumia mkoa.
Akizungumzia upande wa changamoto, Mh. Gallawa ameuomba Mfuko wa Bima ya Afya kufikiria kupunguza riba ya mikopo kwa vituo vya afya ili kuvipatia fursa ya kuweza kukopa vifaa tiba. Hii imetokana na riba ya sasa kuwa kubwa na kupelekea vituo hivyo kushindwa kukopa.
Wakati huo huo, Wananchi wametakiwa kuwa na mapenzi mema na nchi yao katika kuisaidia serikali katika kutekeleza mipango yake ya kuboresha huduma ya afya. Aidha watu binafsi, mashirika na taasisi mbalimbali zimeombwa kuiga mfano wa NHIF katika kutoa msaada wa vifaa tiba.