Wabunge waitaka Serikali ipunguze matumizi!

Wabunge wakiendelea na shughuli za bunge mjini Dodoma.


Na Mwandishi wa Thehabari, Dodoma

BUNGE la bajeti ya Serikali ya mwaka 2011/2012 linaendelea leo mjini hapa baada ya mapumziko ya wiki, huku wabunge wakiishawishi Serikali kupunguza matumizi ya fedha za umma.

Wabunge mbalimbali mbao hadi sasa wamechangia katika bajeti hiyo tangu wiki iliyopita wanaonekana kuitaka Serikali kuhakikisha inapunguza matumizi ikiwa ni njia ya kubana matumizi. Hata hivyo tumeshuhudia baadhi ya wabunge wakipigana vijembe vikali wakati wakichangia bajeti hiyo kiasi cha kumlazimu Mwenyekiti wa Bunge kutumia muda mwingi kuomba wabunge waache malumbano.

Tangu kuanza kwa majadiliano ya bajeti ya Serikali wachingiaji wamekuwa wakitoa maoni mbalimbali ambayo yanalenga kuiboresha bajeti hiyo ambapo kwa upande wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wao wamekuwa wakiunga mkono licha ya kuikosoa katika maeneo machache wakati wa wabunge wa CHADEMA wao hawaiungi mkono bali bajeti mbadala ya kambi ya upinzani ndio wamekuwa wakiiunga mkono.

Mambo mengi yamezungumzwa na wabunge ambao wamechangia katika bajeti hiyo ambapo baadhi ya wabunge kutoka vyama vyote vya siasa ambao wamechangia bajeti hiyo wamekuwa wakiiomba Serikali kusimamia fedha za umma ili kuhakikisha zinatumika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Kwa upande wa wabunge wa CCM pamoja na kuiunga mkono bado wametoa maoni yao katika kuhakikisha bajeti hiyo inamkomboa Mtanzania wa kawaida kama ambavyo Serikali imedhamiria kuwafanya wananchi wake kuwa na unafuu wa maisha.

Wakichangia katika bajeti hiyo baadhi ya wabunge hao wa CCM wamemtaka Mkulo kuhakikisha kuwa vipaumbele ambavyo vimepewa umuhimu katika bajeti hiyo vinatekekezwa kwa vitendo na si kuishia katika vitabu vya bajeti.
Pia wameitaka Serikali kuweka mkazo katika ukusanyaji wa mapato kwa kutafuta vyanzo vipya vya ukusaji wa mapato ili kufanikisha kutokuwa na bajeti ya Serikali ambayo inakuwa inategemea wahisani.

Wakati kwa upande wa wabunge wa upinzani licha ya kutoaiunga mkono bajeti hiyo wamekuwa wakitoa maoni yao kwa kuitaka Serikali kumaliza matatizo ambayo yanawakabili wananchi wake huku wakitaka huduma muhimu za jamii ziboreshwe kwa vitendo.

Wakati wanachangia pamoja na mambo mengine wamekuwa wakilalamikia matumizi mabaya ya fedha za umma ambapo walisema kuna fedha nyingi za umma zinapotea kutokana na kukosekana kwa usimamizi mzuri wa fedha hizo.
Wakati wanachangia bajeti hiyo wabunge hao wa upinzani wamekuwa wakiitaka Serikali kuwa na utaratibu unaoleweka katika kununua magari ya mawaziri na watumishi wa ngazi za juu wa umma ambapo wanataka badala ya kutumia mashangingi sasa wawe wanauizwa magari kila baada ya miaka mitano.