PAMOJA na masuala ya kiuchumi wajumbe zaidi ya 2500 kwenye kongamano hilo la siku tano watajadili pia masuala ya ulinzi wa mazingira na ya maradhi. Wakuu wa serikali na viongozi wa nchi karibu 50 wanatarajiwa kulihudhuria kongamano la mjini Davos kwa lengo la kuhimiza matumaini na kuimarisha imani juu ya uchumi wa dunia, hasa wakati huu ambapo matumaini ya ustawi yamejitokeza.
Wadau zaidi ya 2000, kutoka tasnia za uchumi, mazingira, biashara na afya watajadiliana juu ya njia za kuuelekeza uchumi wa dunia katika mkondo wa ustawi na kuudumisha. Kongamano la mwaka jana katika mji huo wa Davos nchini Uswisi lilifanyika wakati bara la Ulaya lilipokuwa linakabiliwa na mgogoro mkubwa wa madeni.
Mgogoro huo ulitishia kuitoa Ugiriki nje ya Umoja wa sarafu ya Euro. Hata hivyo kongamano la mwaka huu linafanyika katika muktadha wa matumaini ya tahadhari. Matumaini ya kumaliza mgogoro wa kiuchumi.
Mwanzilishi wa kongamano hilo, Klaus Schwab amewataka washiriki waufungue ukarasa mpya, baada ya mgogoro wa madeni wa barani Ulaya uliosababisha mshuko wa uchumi duniani.
Akilifungua kongamano hilo mwasisi huyo Schwab aliwaambia wajumbe:”anatumani wataondoka kwenye mkutano huu wakiwa na mtazamo uanovuka njia za kuidhibiti migogoro ”
Schwab amewataka washiriki wawe na moyo wa matumaini badala ya kuishia katika njia za kuikabili migogoro. Hata hivyo idadi kubwa ya washiriki wamesema wanayo matumaini juu ya uchumi wa dunia.
Miongoni mwa washiriki mashuhuri kwenye kongamano la mjini Davos ni Waziri Mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev ambae aliwahutubia wajumbe na kuwapa taarifa juu ya ustawi wa uchumi wa asilimia 3.5 nchini mwake. Mkuu wa Benki Kuu ya Ulaya Mario Draghi atazungumzia juu ya changamoto zinazokuja.Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa Christine Lagarde pia anashiriki katika kongamano la Davos, nchini Uswisi.
-DW