Lengo la SMZ ni Kukuza Kipato cha Mwananchi- Dk Shein

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (katikati) akimkabidhi Cheti cha Shukurani Bibi Nuru Hafidhi Mzee, mstaafu katibu Muhtasi Wizara ya
Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika wakati wa sherehe za Kilele cha Wiki ya Uwezeshaji wananchi Kiuchumi katika Ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Zanzibar (kushoto) Waziri wa Kazi, Uweshaji, Wananchi Kiuchumi na Ushirika Haroun Ali Suleiman.[Picha na Ramadhan Othman, IKULU]


Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia vyama vya ushirika na vikundi vya wajasiriamali zina lengo la kuwaongezea kipato na kukuza uchumi.

Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar katika maadhimisho ya kilele cha ‘Wiki ya Uwezeshaji’ yaliyohudhuriwa na mamia ya Wajasiriamali kutoka vikundi mbali mbali vya Unguja na Pemba. Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi hizo za makusudi ili hatimae wananchi waweze kujiajiri na kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kufarajika kwake na kuona utaratibu mzuri wa Mfuko wa Zakka kuwa umeanza vizuri na kuna vikundi ambavyo tayari vimebahatika kuzipatia fedha hizo kwa awamu ya kwanza.

“Napenda niwatoe wananchi wasiwasi kuwa utaratibu huu utakuwa endelevu na hivyo wale ambao hawakubahatika kwenye awamu hii, Inshaallah Mwenyezi Mungu akitujaalia watapata katika awamu zinazofuata,” alisema Dk. Shein.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, (katikati) akimkabidhi Fatma Abdalla Issa, wa Kikundi cha “Tanaweza Coop” Ole Kaskazini Pemba, Mfano wa Cheki ya Shilingi za Kitanzania Millioni Mia tatu na Laki Saba kwa niaba ya Vikundi vya Ushirika na Wajasiriamali wa Mikoa Mitano ya Zanzibar wakati wa sherehe za Kilele cha Wiki ya Uwezeshaji wananchi Kiuchumi katika Ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Zanzibar (kushoto) Waziri wa Kazi, Uweshaji, Wananchi Kiuchumi na Ushirika Haroun Ali
Suleiman. [Picha na Ramadhan Othman, IKULU]


Aidha, Dk. Shein alisema kuwa suala la uwezeshaji linajumuisha vitendo na hatua za makusudi zinazochukuliwa na Serikali kwa ajili ya kukuza na kuendeleza ujuzi na ubunifu wa shughuli za kiuchumi na maarifa ili kuwawezesha wananchi kujiajiri.

Alisema kuwa lengo ni kuwa mtu aweze kuongeza tija na kukinyanyua kipato chake ambapo Serikali inakusudia kumfanya mtu ajitegemee kwa kutumia fursa zilizopo sanjari na kutumia maarifa yake na rasilimali zilizomzunguka ataweza kujipatia kipato au ajira na hivyo ataweza kuondokana na umasikini na kupunguza utegemezi kwa wengine.

Hivyo, Dk. Shein alisema kuwa juhudi kadhaa zinazofanywa na Serikalui zikiwezo hizo za kuanzisha Mifuko mbali mb ali ya kusaidia kuwawezesha wananchi zinaazma hiyo.

Aliwataka kuongeza ari, kwani ari ni tabia ya kiungwana na kuzitunza fursa wanazozipata kikamilifu ili kwa pamoja kuweza kuijenga Zanzibar mpya yenye matumaioni na fursa za kutosha za ajira za staha na zenye tija. “Wajasiriamali mkipewa fursa Mnaweza”malisisitiza Dk. Shein.

Kwa upande wake Waziri wa Wizara hiyo alitoa shukurani na pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa maelekezo na miongozo yake kwa Wizara hiyo ambayo ndio iliyopelekea kupata mafanikio makubwa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi Asha Ali Abdalla, alisema kuwa wiki ya uwezeshaji ilianza kuadhimishwa mwaka 2011 kama sehemu ya mikakati ya Wizara katika kutoa hamasa kwenye masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Alisema kuwa Wizara hiyo imetoa jumla ya mikopo 195 kwa Unguja na Pemba yenye thamani ya Tsh. 143,000,000 kwa Wajasiriamali kupitia mfuko wa kujitegemea pia, kwa kushirikiana na benki ya Watu wa Zanzibar jumla ya mikopo 19 ya kuendelezwa yenye thamani ya Shs. 62,944,831 imetolewa kupitia mfuko wa JK/AK.

Aidha, Katibu huyo alisema kuwa taalamuma ya ujasiriamali kwa wajasirialami wadogo wadogo 94 imetolewa ikiwa ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa kuwasaidia vijana kujenga tabia ya kupenda kazi na kujiajiri ambapo jumla ya vijana 30 walipatiwa taaluma iliyolenga kubadilisha mitazamo yao juu ya kazi.

Katibu Mkuu huyo alisema kuwa SACCOS Benki 5 mpya zimeanzishwa na nyengine 11 zimeimarishwa na kupatiwa mafunzo ili ziweze kutoa huduma bora za kifedha kwa wajasiriamali na watumishi. Pia alisema kuwa jumla ya Shs milioni 303, 7000,000 zilizotolewa na Wizara hiyo ambapo ziligawiwa kwa vikundi vya ushirika 177.

Mapema Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Sheikh Abdallah Talib, alisema kuwa Shs milioni 505,399,009 zimetolewa na waumini 17 waliochangia katika mfuko huo wa Zakka ambapo vikundi 188 na watu 145 wamenufaika katika awamu ya kwanza ya ugawaji.

Alisema kuwa fedha hizo zimegawiwa kwa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananachi Kiuchumi na Ushirika, vikundi vya Wajasiariamali, Jumuiya za Wawake Kiislamu, Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Jumuiya za Kuhifadhi Quran, Umoja wa Watu wenye ulemavu, walioathirika na madawa ya kulevya na wengineo.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alikabidhi mfano wa cheki ya Shs. Milioni 303,7000,000 kwa wenyeviti wa vikundi vya Wajasiriamali Unguja na Pemba ambapo pia, Vyeti vya Shukrani pamoja na fedha taslim kwa Washindi walioandika Mpango mzuri wa biashara zilitolewa na wafanyakazi wastaafu wa Wizara hiyo nao walikabidhiwa zawadi zao.