KATIKA wiki za hapa karibuni kumekuwa na mijadala na mazungumzo mengi kuhusu mikakati ya maendeleo ya mikoa ya Kusini hususan Mkoa wa Mtwara. Mazungumzo hayo yamekuwa na lugha kali na yameambatana, hatimaye, na maandamano na mikutano ya hadhara. Kiini chake ni matumizi ya gesi iliyogunduliwa mkoani kwa ajili ya miradi au mipango ya maendeleo ya mkoa huo, mipango iliyopo mbioni kutekelezwa au inayotarajia kutekelezwa. Mwenendo wa mazungumzo, maandamano na mikutano ya hadhara imeelekea kuashiria shari na kuvunjika kwa amani.
Aidha vituko na kauli hizo zimekaribia kujenga kutokuelewana kati ya Viongozi wa Vyama vya Siasa na Serikali, kati ya wanachama wa vyama vya siasa na viongozi wao, kati ya wananchi na viongozi wa Serikali. Mtafaruku huu haufai kuachwa uendeleee na kutishia usalama. Mipango ya maendeleo siyo Siri. Mikakati na mbinu za Utekelezaji wake siyo Siri. Maelezo yake mazuri yanaweza kutolewa yakadhihirisha namna na kasi ambayo raslimali zitawanufaisha wananchi wa eneo zilizomo na Taifa zima. Utekelezaji wa miradi unategemea masharti kadhaa, k.m. Uwapo wa mitaji na teknolojia. Lakini pia mwekezaji, awe Serikali au Sekta binafsi, atataka iwepo hali ya utulivu na usalama wa watu, hali na mali. Hayo yatadaiwa na wawekezaji wa ndani na wa nje. Vurugu, fujo, vitisho havivutii uwekezaji.
Nikiwa Mwana Mtwara na raia mwema mpenda nchi, nimefadhaishwa sana na matukio haya ya siku za karibuni Mtwara. Kwa sababu hiyo natoa wito kwa wadau wote wa maendeleo ya Mtwara kusitisha harakati hizi na maandamano na mihadhara na badala yake wajipange KUKAA PAMOJA katika meza moja, kupitia historia, kutathmini mipango, kuchambua kwa kina mikakati ya utekelezaji wake, na hatimaye kufikia muafaka wa Ujia wa maendeleo. Fujo, vitisho, kupimana nguvu na malumbano kamwe si masharti ya maendeleo. Mazungumzo yataboresha sera, ya uwekezaji ya mkoa na nchi.
Linalowezekana leo lisingoje kesho.
Benjamin William Mkapa
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania