Dk Shein ‘Tunaendelea Kuvifufua na Kuvikuza Viwanda’

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akifungua Mkutano wa Saba (7) wa Baraza la Biashara la Zanzibar ZBC,uliofanyika leo katika Ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja,(kulia) Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk.Abduhamid Yahaya Mzee,na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko,Nassor Ahmed Mazrui,[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali inaendelea kujenga mazingira mazuri yatakayopelekea kuvifufua na kuvikuza viwanda hasa viwanda vidogo vidogo ili viweze kutoa mchango katika soko la ajira na kuinua mchango wake katika Pato la Taifa.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar katika ufunguzi wa Mkutano wa saba wa Baraza la Biasahara la Zanzibar (ZBC),ambapo Dk. Shein alikuwa ni Mwenyekiti wa Mkutano huo.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa serikali inatambua umuhimu wa kuwa na viwanda ili kuongeza vyanzo vya mapato, ambapo kwa mwaka wa fedha 2011/2012 mchango wake katika Pato la Taifa la viwanda ulifikia asilimia 3.9, ambayo ipo haja ya kuimarishwa zaidi.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kuimarisha sekta ya viwanda na jiytihada za kuitekeleza zimeshaanza ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwepo kwa huduma za umeme wa uhakika, kuimarisha miundombinu ya barabara, bandari, uwanja wa ndege na mawasiliano.Alisisitia kuwa washirika wa sekta binafsi na wao watashiikishwa ili watoe michango yao,uzoefu wao na hatie kueleza matarajio yao katika kulifanikisha jambo hilo huku akisisitiza umuhimu wa mchango wa sekta binafsi katika kufanikisha suala zima la maendeleo ya viwanda hapa nchini.
Dk. Shein alisema kuwa Mkutano huo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kushirikisha sekta binafsi katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar na ustawi wa wananchi kwa kuzingatia rasilimali zilizopo.Katika mkutano huo, wa saba wenye maudhui ya ‘Ubia na Uwekezaji kwa Maendeleo ya Viwanda, Zanzibar’, ambapo maudhui hayo yaliopelekea kuchaguliwa mada zitakazowasilishwa kwenye kikao hicho cha siku moja.
“ Nina imamni kuwa sote tutakubaliana kuwa viwanda vina umuhimu mkubwa kwa maendleo ya uchumi wa nchi yetu na kuwapunguzia changamoto ya ajira kwa wananchi wetu”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa lengo la serikali la kufanya utalii uwe na manufaa kwa wananchi wote katika dhana ya ‘utalii kwa wote’.
Kutokana na hali hiyo Dk. Shein alieleza kufarajika kwake kwa kuona kuwa wananchi wameufahamu vizuri umuhimu wa utalii kwa maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii na kwamba itihada zaidi zitaendelea kwa ajili ya kuwafahamisha zaidi.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa uwekezaj katika ujenzi wa mikahawa na mahoteli ya daraja mbali mbali ya kuwahudumia watalii umeongezeka.
Hta hivyo, alieleza kuwa bado kuja haja ya kuimarisha ushirikia katika shughuli mbali mbali za utalii pamoja na kuimarisha utalii wa ndani, kwani bado haujapewa umuhimu unaotahiki.
Dk. Shein aliwahakikishia wajumbe na wageni waalikwa waliohudhuria mkutano huo pamoja na wananchi kwa ujumla kuwa Serikali anayoiongoza itaendelea kuipa nguvu Kamisheni ya Utalii ili iweze kufanya kazi kwa kasi zaidi.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitoa shukurani kwa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Biashara la Zanzibar, likiongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa kazi nzuri wanayofanya pamoja na maandalizi mazuri ya Mkutano huo.
Pia, alitoa shukurani kwa wajumbe wa Baraza la Taifa la Biasahra Tanzania (TNBC) kutoka Dar-es-Salaam kwa ujio wao wa kushiriki katika mkutano huo na kusisitiza kuwa uwepo wao ni kielelezo cha ushirikiano mzuri uliopo katika utekelezaji wa majukumu.
Nae Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe. Nassor Ahmed Mazrui alileza kuwa suala la viwanda lina umuhimu mkubwa sana katika kuimarisha uchumi sambamba na kupanua soko la ajira hapa Zanzibar.
Mhe. Mazrui alisema kuwa suala la ajira zinazotokana na viwanda hapa Zanzbar bado ni dogo sana sanjari na pato la Taifa linalotokana na viwanda nalo bado kuwa dogo kwa upande wa Zanzibar ikilinganishwa na nchi yengine za visiwa kama Zanzibar.
Nao wajumbe wa Mkutano huo walieleza haja ya mashirikino ya pamoja kwa taasisi za serikali na taasisi binafsi kwa lengo la kuimarisha sekta hiyo ya viwanda hapa nchini.
Katika Mkutano huo viongozi mbali mbali walihudhuria wakiwemo viongozi wa Serikali pamoja na kutoka sekta binafsi, miongoni mwa viongozi wa serikali waliohudhuria ni pamoja na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.