JK Amtembelea Manumba Hospitali

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi (DCI), Kamishna Robert Manumba

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete Januari 17, 2013, amemtembelea hospitali Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini, Bwana Robert Manumba na kumjulia hali ambaye amelazwa kwenye Hospitali ya Aga Khan mjini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema kwenye hospitali hiyo, Rais Kikwete amejulishwa na uongozi na madaktari kuwa bado hali ya afya ya Bwana Manumba inahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari na wauguzi.

Juzi vyombo vya habari viliripoti kuwa hali ya ya Manumba ni mbaya na amelazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam. Habari zilizopatikana zilieleza kuwa Manumba amelazwa hospitalini hapo baada ya kusumbuliwa na maradhi kadhaa, ikiwamo figo.

Taarifa za ndani kutoka Jeshi la Polisi zilisema juzi hali ya kiongozi huyo haikuwa nzuri baada ya kuugua malaria ghafla na hali hiyo ilisababisha pia figo zake zote mbili kushindwa kufanya kazi.