Wanaoomba Uongozi TFF Wafikia 45

Rais wa TFF, Leodger Tenga

WANAMICHEZO 45 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utakaofanyika Februari 24 mwaka huu. Nafasi zinazowaniwa ni Rais, Makamu wa Rais na wajumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda 13 tofauti.

Waombaji wapya 11 waliojitokeza Januari 18 mwaka huu ni Richard Rukambura anayeomba urais wakati kwa upande wa ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Kaliro Samson, Jumbe Magati, Richard Rukambura, Omari Walii, Ahmed Mgoyi, John Kiteve, Stanley Lugenge, Francis Ndulane, Riziki Majara na Hassan Othuman Hassanoo.

Mwisho wa kuchukua fomu kwa waombaji wote ni Januari 18 mwaka huu saa 10 kamili alasiri. Fomu pia zinaweza kuchukuliwa katika tovuti ya TFF ambayo ni www.tff.or.tz na kurejeshwa kupitia email ya tfftz@yahoo.com Pia Kanuni za Uchaguzi za TFF zinapatikana katika tovuti hiyo.

Orodha kamili ya waombaji ni Athuman Nyamlani, Jamal Malinzi, Omari Nkwarulo na Richard Rukambura (Rais). Walioomba kuwania nafasi ya Makamu wa Rais ni Michael Wambura, Ramadhan Nassib na Wallace Karia.

Kwa upande wa ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Salum Chama na Kaliro Samson (Kagera na Geita), Jumbe Magati, Mugisha Galibona, Richard Rukambura, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza).

Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo, Elly Mbise na Omari Walii (Arusha na Manyara), Ahmed Mgoyi na Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Blassy Kiondo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa) na James Mhagama na Stanley Lugenge (Njombe na Ruvuma).

Athuman Kambi, Francis Ndulane na Zafarani Damoder (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi, Geofrey Nyange, Hassan Othman Hassanoo, Riziki Majara na Twahili Njoki (Morogoro na Pwani), Elias Mwanjala, Eliud Mvella na John Kiteve (Iringa na Mbeya), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Omari Abdulkadir na Shaffih Dauda (Dar es Salaam).

Wakati huo huo; Waombaji watatu wapya wamejitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) ambayo uchaguzi wake utafanyika Februari 22 mwaka huu.

Walioingia leo (Januari 18 mwaka huu) kwenye kinyang’anyiro hicho ni Hamad Yahya wa Kagera Sugar anayeomba uenyekiti wakati Christopher Peter wa Moro United na Kazimoto Miraji Muzo wa Pamba ya Mwanza wanaoomba ujumbe wa Bodi kuwakilisha klabu za Ligi Daraja la Kwanza.

Orodha kamili ya waombaji uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu ni Hamad Yahya wa Kagera Sugar na Yusuf Manji wa Yanga wanaoomba uenyekiti wakati Makamu Mwenyekiti aliyeomba ni Said Mohamed wa Azam. Kwa upande wa wajumbe wawili kuwakilisha klabu za Daraja la Kwanza ni Christopher Peter Lunkombe wa Moro United ya Dar es Salaam na Kazimoto Miraji Muzo wa Pamba ya Mwanza.