Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete atahudhuria mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika Wanachama wa Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) ambapo ripoti ya Tanzania itajadiliwa. Rais alithibitisha kuhudhuria mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Januari 26 jijini Addis Ababa Ethiopia mara baada ya mazungumzo yake na ujumbe wa APRM Tanzania yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam Alhamisi.
Katika mazungumzo hayo Rais Kikwete alieleza kufurahishwa kwake na namna mchakato wa APRM ulivyosimamiwa hapa nchini na kulipongeza Baraza la Usimamizi la Taifa la APRM na Sekretarieti yake kwa kazi nzuri.
“Nawapongeza Baraza na Sekretarieti ya APRM Tanzania kwa kusimamia na kuendesha mchakato huu wa APRM hapa nchini kwetu kwa ufanisi na kujituma sana. Sasa name niko tayari kwenda kukutana na wenzangu kuiwasilisha ripoti yetu kama ilivyopangwa,” alisema Rais Kikwete.
Katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye wizara yake ndiyo inayoratibu shughuli za APRM alimweleza Rais kuwa kukamilika kwa ripoti atakayoiwasilisha Addis Ababa ni matokeo ya zoezi lililoshirikisha wadau wengi wa utawala bora nchi na kusimamiwa na cgombo huru cha APRM Tanzania.
“Ripoti yenyewe kwa ujumla ni utafiri uliosheheni weledi. Ni ripoti ambayo uimeichambua nchi yetu kwa haki; ikiainisha maeneo tunayofanya vyema na maeneo ambayo nchi yetu ina changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi,” alisema Waziri Membe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi la Taifa la APRM, Prof. Hasa Mlawa alimweleza Rais Kikwete kuwa uwasilishaji wa ripoti ya Tanzania jijini Addis utatanguliwa na zoezi kama hilo kwa nchi ya Zambia.
“Ratiba tuliyopewa kutoka makao makuu ya APRM inaonesha kuwa uwasilishaji wa ripoti ya Tanzania utatanguliwa na wenzetu wa Zambia,” alisema na kumhakikishia Rais kuwa mchakato wa APRM hapa nchini ulifanyika kwa kufuata vigezo vyote vinavyokubalika kiutafiti.
Mchakato wa APRM kwa sasa unahusisha nchi 31 kati ya 54 za Afrika na uliassiiwa mwaka 2003 na wakuu wan chi za Afrika kwa ajili ya kuchagiza utawala bora kwa kushirikisha wananchi wenyewe kushauriana na Serikali zao.