SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Baraza la Sanaa la Taifa, imebariki kufanyika kwa Fainali za Taifa za Miss Utalii Tanzania 2012/13 baada ya kuridhishwa na maandalizi yaliyofanywa na Miss Tourism Tanzania Organisation waandaaji wenye dhima ya kikomo ya kuandaa na kuendesha mashindano hayo kitaifa na kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Rais Miss Tourism Tanzania Organisation, Erasto Gideon Chipungahelo amesema ruhusa hiyo imetolewa kwa kuzingatia sheria za nchi, kanuni na taratibu za mashindano.
Alisema Serikali pia imeridhishwa na jinsi Fainali za ngazi za mikoa na kanda zilivyofanyika kwa mafanikio, ambapo kila mkoa umepata washindi wenye sifa za kuwakilisha mkoa husika katika Fainali za Taifa mwaka huu.
Aidha ameongeza kuwa jumla ya warembo 60 wanaingia rasmi kambini kesho katika hoteli ya Ikondelelo Lodge Dar es Salaam, kuanza mbio za kuwania Taji hilo la Taifa.
Washindi wa 1-5 wa Fainali za Taifa, watawakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya Dunia yakiwemo ya International Miss Tourism World, Miss Tourism United Nation, Miss Heritage World, Miss Tourism University World, Miss Globe International na wengineo.
“Miss Utalii Tanzania, hadi sasa tunashikilia Jumla ya mataji 5 ya Dunia na kimataifa, yakiwemo ya Miss Tourism World 2005-Africa, Miss Tourism World 2006-SADC, Miss Tourism World 2007- Africa, Miss Tourism Model Of The World 2008-Personality n.k,” alisema Rais katika taarifa hiyo.
Fainali za Taifa mwaka huu zimepangwa kufanyika wiki ya kwanza ya Februari wilaya ya Temeke na mkoa wa Dar es Salaam ukiwa umepewa heshima ya kuwa wenyeji wa Fainali hizo.