Sina Jema la Kujifunza kwa Wazee Hawa!

Tumeonewa kiasi cha kutosha

Wapenda, kheri ya mwaka 2013.

DUU, kwa hakika kuna kazi katika Taifa letu. Kumbe Mzee Gwao, naye ni kada mahiri? Nakumbuka ule ujanja ujanja wake wa kutaka wauziwe nyumba pale Upanga. Akajifanya mzalendo kweli kweli, kumbe alikuwa amewekwa front na wadosi. Akashitukiwa.
Gazeti la Nipashe likaanika alivyo na nyumba kuanzia Msasani hadi Chang’ombe, na maelfu ya dola anayolipwa kila mwezi kutoka kwa wapangaji wake; ilhali yeye akiendelea kuishi ‘bure’ katika nyumba za NHC. Nchi hii ina mambo.

Ukitoka kwa Gwao unakwenda kwa Iddi Simba. Mzee wa Wazee wa Dar es Salaam. Huyu kalamba Shilingi zaidi ya milioni 300 kutoka kwa Kisena (UDA). Zikaingizwa moja kwa moja kwenye akaunti yake. Breki yake ya kwanza baada ya kuzipata ni kwenda kupata shangingi (Land Cruiser) la kisasa kabisa kwa bei mbaya. Anakula kiyoyozi. Huyu ndiye mzee anayetaka kutufundisha vijana tabia njema na uadilifu kwa Taifa.

Kutoka hapo nakwenda moja kwa moja kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mzee wangu Madabida. Yeye baada ya kuona juhudi zote za kuongeza ukwasi zinalegalega, akaamua kutengeneza ARV’s feki.

Zikajazwa unga wa muhogo! Waathirika kila walipozibugia , wakajikuta hali zao zikizidi kwenda mrama! Zawadi pekee kwa wana CCM Mkoa wa Dar es Salaam waliyoamua kumpa kutokana na maangamizi kwa wagonjwa wa Ukimwi, ni kumpa u-nahodha wa kukiongoza Chama katika mkoa mnene na mzito kabisa – Dar es Salaam.

Nasikia mafunzo ya JKT yanarejeshwa ili kuwapa uzalendo Watanzania. Sina hakika, lakini nadhani hawa wote walipita, ama JKT, au Magogoni. Kama hivyo ndivyo, sioni JKT mpya itakuja na jipya gani zaidi ya kutufunza matumizi ya silaha!

Kwangu mimi, sina jema la kujifunza kutoka kwa wazee hawa.

Manyerere Jackton
Dar es Salaam