Spika wa Bunge kikaangoni, Chadema wamgeuka

Na Mwandishi wa Thehabari, Dodoma
 
HATUA ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kumkingia kifua Waziri Mkuu wa Tanzania alipokuwa kujibu baadhi ya maswali bungeni kwenye kipindi cha maswali ya papo hapo kwa waziri mkuu imemponza Spika Makinda.
Hali hiyo imekuja baada ya Kambi ya Upinzani Bungeni kuchukua uamuzi    wa kumfikisha Makinda katika Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge ili uamuzi wake wa kumkataza Waziri Mkuu Mizengo Pinda asijibu maswali kuhusu mauji ya eneo la Nyamongo mkoani Tarime yalioulizwa na wabunge wa upinzani ujadiliwe na kutolewa maamuzi kama ni haki.
Kambi ya upinzani imechukua hatua hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu kumuuliza Waziri Mkuu swali la mauaji hayo na Makinda akapinga lisijibiwe kwa kuwa suala hilo lipo mahakamani na Lisu mwenyewe yupo nje kwa dhamana.
Akitoa uamuzi huo wa Kambi ya Upinzani Bungeni jana mjini hapa, Mnadhimu Mkuu, Kambi Rasmi ya Upinzani ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki Lissu alisema tayari wameandaa hati ya ushahidi wa kutosha kuhusu uamuzi tata ambayo yamekuwa yakifanywa na Makinda katika nafasi yake ya Uspika.
“Kambi ya rasmi ya upinzani bungeni inasikitishwa na namna ambavyo Spika wa Bunge amekuwa akishughulikia mijadala ya masuala muhimu kwa umma na ambavyo yanaelekea kuibua mzozo katika utendaji wa Serikali na watendaji wake wakuu.
“Hii inafuatia uamuzi wa Spika kukataa maswali aliyoulizwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu mauwaji ya wananchi wengi wa vijiji vinavyozunguka mgodi wa dhahabu wa North Mara katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime  yaliyofanywa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Polisi Tarime na Rorya kwa vipindi tofauti tangu mwaka 2008,” alisema Lissu.
Tunashangaza kwanini Spika Makinda alikataza maswali hayo yasijibiwe kwa hoja kwamba yalikuwa yanahusu mambo ambayo tayari yako mahakamani na kwa hiyo kuyajadili bungeni itakuwa sawa na kuingilia uhuru na mamlaka ya Mahakama kinyume na kanuni 64(1)(c) ya kanuni za kudumu za Bunge, 2007.
“Alipoombwa mwongozo wake kutokana na ukweli kwamba hakuna kesi hata moja ambayo imefunguliwa au inayoendelea katika mahakama yoyote ya Tanzania inayohusu mauji ya wananchi wa Nyamongo au yanayowahusu Polisi wanaohusika na mauji hayo. Spika alidai waulizaji maswali wenyewe walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya jinai katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime,”alisema Lissu.
Kutokana na hali hiyo alisema Kambi ya Upinzani Bungeni imefikia uamuzi wa kuandika hati hiyo yenye ushahidi wa kutosha na kwamba jana mchana walikuwa wameikabidhi kwa Katibu wa Bunge Dk. Thomas Kashilila ili aweze kuipeleka katika Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge ili Makinda aweze kuchunguzwa kwa uamuzi wake huo.
“Kambi ya Upinzani imeamua kuchukua uamuzi wa kumpeleka Makinda kwa Kamati ya Kanuni za Bunge, ili aweze kujadiliwa na kisha kupata ufumbuzi ambao utaweza kusaidia kutendeka kwa haki pindi Spika anapokuwa akisimamia vikao vya Bunge.
“Ni uamuzi mgumu kuamua kumfikisha Spika katika kamati hiyo maana ni sawa na kuhoji uadilifu wake ama uwezo wake lakini tumeamua kufanya hivyo ili kuhakikisha anajadiliwa na hatimaye kuwa na Spika ambaye atakuwa anatoa haki na kufanya maamuzi ya kibunge bila kupindisha kanuni zilizopo kwa maslahi ya Taifa,” alisema Lissu.
Alisema wana matumani makubwa na kamati ambayo itamjadili Makinda kwani itafanya kazi zake na kutoa maamuzi bila kuwa na upendeleo wowote ule lakini akaweka bayana kuwa wakati wa kamati itakapokaa Makinda na Naibu Spika Job Ndugai hawataruhusiwa kuwa katika nafasi zao kwa kuwa Spika ndio mwenyekiti na naibu wake ni makamu mwenyekiti wa kamati hiyo.
Lissu alitumia nafasi hiyo kudai kuwa Spika Makinda amekuwa akikiuka kanuni za kudumu za Bunge na kwamba kwa mujibu wa kanuni hizo,Spika wa Bunge ana mamlaka makubwa kimaamuzi hata hivyo Spika hawezi akaendesha Bunge kama anavyoona yeye binafsi.
Anatakiwa kuzingatia kanuni anazotakiwa kutoa muda wote ni kanuni ya nane inayomtaka kuendesha Bunge kwa kutoa maamuzi kwa haki, uadilifu na kanuni nyingine zilizopo. Alitumia nafasi hiyo kusisitiza kuwa licha ya kufanyika mauji hayo ya Nyamongo hakuna kesi yoyote ambayo imefunguliwa inayohusu mauji hayo hivyo kitendo cha Makinda kukataza Waziri Mkuu asijibu maana yake ni kumkingia kifua na wao hawatakubali kuona hali hiyo ikiendelea kwani kuna matukio makubwa yanayotokea ambayo yanahitaji kuzungumzwa Bungeni lakini yanakataliwa bila sababu.
Aliongeza kuwa Makinda amekuwa akiwabebea zaidi mawaziri kwa kutaa wasijibu hoja ambazo wanaulizwa Bungeni na hata ikitokea waziri amedanganya Bunge hakuna hatua ambazi zinachukuliwa ambapo alitumia mfano wa ripoti ya mauji ya Arusha ambayo Mbunge wa Arusha Mjini Godbles Lema aliwakilisha kwa Spika lakini hadi leo hakuna hatua zilizochukuliwa ama kutolewa taarifa hiyo kwa umma.