Vijana Waaswa Kutotumiwa Kuvuruga Amani Nchini

“Nawasihi vijana wote msibabaishwe na wala msiyumbishwe na mtu au kundi lolote linaloweza kuwagawa, nawaomba muwe macho,imara na thabiti katika kulinda na kutetea mafanikio yaliyopatikana”

Na Aron Msigwa – Maelezo Zanzibar

VIJANA nchini wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuwa mstari wa mbele kulinda amani, utulivu na mafanikio makubwa yaliyoachwa na waasisi wa taifa la Tanzania na kuepuka kutumiwa na watu au kundi lolote kuvunja sheria za nchi na kuvuruga amani iliyopo.

Kauli hiyo imetolewa mjini Zanzibar na Waziri wa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana, Wanawake na watoto Bi. Zainab Omar Mohammed wakati wa mkutano wa tathmini ya mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2012 unaowahusisha viongozi na na waratibu wa mbio hizo kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania bara na Zanzibar.

Amesema vijana kote nchini wanawajibu wa kufanya kazi kwa bidii na kulinda mafanikio makubwa yaliyoachwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume waasisi wa taifa la Tanzania.

Amewataka vijana kukumbuka juhudi kubwa zilizofanywa na waasisi wa taifa la Tanzania katika kupigania uhuru kwa njia ya amani na Mapinduzi pale amani iliposhindikana kutokana na njama za wakoloni.
“Nawasihi vijana wote msibabaishwe na wala msiyumbishwe na mtu au kundi lolote linaloweza kuwagawa, nawaomba muwe macho,imara na thabiti katika kulinda na kutetea mafanikio yaliyopatikana” Amesema.
Bi. Zainab amesema juhudi za wazi zilizofanywa na waasisi zimezaa umoja wa Tanzania ambao hivi karibuni utatimiza miaka 49 ifikapo tarehe 26, Aprili 2013 na kubainisha kuwa umoja huo umekua mfano wa kuigwa na kielezo cha amani kwa Afrika na dunia.

Kuhusu umoja wa watanzania uliopo amesema kuwa umeondoa ubaguzi wa rangi ,kuleta maelewano mazuri baina ya nchi majirani,kukukza lugha ya Kiswahili jambo ambalo limekuwa chachu kubwa ya amani na upendo miongoni mwa watanzania.

Aidha kuhusu kufanyika kwa mkutano huo wa tathmni ya mbio za Mwenge kwa mwaka 2012 nchini Bi. Zainab Mohamed amesema kuwa tathmini hiyo inatoa fursa ya kuangalia mapungufu yaliyojitokeza wakati wa mbio hizo na kutafuta namna ya kuyaondoa ili yasijirudie katika shughuli zijazo.
Katika hatua nyingine ametoa wito kwa viongozi wa mikoa na wilaya kusimamia ipasavyo na kutoa taarifa za matumizi ya fedha zinazotolewa na wananchi kuchangia shughuli za maendeleo katika maeneo yao ili kuondoa malalamiko na manunguniko yanayoweza kujitokeza.

“Nawashauri viongozi wa mikoa na wilaya kuhusiana na michango inayokusanywa kutoka kwa wachangiaji mbalimbali ni vizuri kuwapa taarifa jinsi michango yao ilivyotumika kwa vitendo ili kuhakikisha kuwa waliochangishwa wanashiriki moja kwa moja katika mipango ya kuondoa kero zao”
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. James Kajugusi akitoa taarifa ya wizara hiyo kuhusu mbio za mwenge kwa mwaka 2012 na ushiriki wa vijana amesema kuwa vijana ambao ni rasilimali kubwa ya taifa walishiriki kikamilifu katika kufanikisha uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema jumla ya vikundi 104 vya vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini vilipata fursa ya kueleza shughuli mbalimbali wanazozifanya kupitia maonesho ya wiki ya vijana mkoani Shinyanga.
Amesema vijana walipata nafasi ya kujifunza masuala mbalimbali kuhusu matumizi ya takwimu za Sensa ya Watu na Makazi 2012, umuhimu wa Vijana kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, ushiriki wa Vijana katika mabadiliko ya Katiba na ushiriki wa vijana wahitimu wa vyuo vikuu na mchango wao katika kuleta maendeleo ya nchi.

Bw. Kajugusi ameeleza kuwa mbio hizo kwa mwaka 2012 zilihusisha pia mapambano dhidi ya matumizi ya madawa ya kulevya, Rushwa na mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ampapo wananchi 2363 mkoani shinyanga walijitokeza kupima afya zao wanawake wakiwa 960 na wanaume 1403.
Amesema katika zoezi hilo watu 40 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU wanaume 17 na wanawake 23 jumla ya maambukizi ikiwa asilimia 1.75%. Pia ameeleza kuwa katika wiki ya vijana iliyofanyika mkoani shinyanga wananchi walihamasishwa kushiriki katika zoezi la hiari la la uchangiaji wa damu ambapo kiasi cha damu lita 342 zilipatikana.