RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Januari 12, 2013, amezindua shule mpya na ya kisasa kabisa ya Sekondari ya Mlimani-Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwenye pwani ya kaskazini ya Zanzibar.
Uzinduzi wa shule hiyo yenye majengo na huduma za kisasa ikiwa ni pamoja na maabara za masomo ya fikizia, kemia, biolojia na kompyuta ni sehemu ya Sherehe za Miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo sherehe zake zimefanyika kwenye Uwanja wa Amaan, mjini Zanzibar, na kuhudhuriwa na Rais kikwete.
Shule hiyo iliyogharimu kiasi cha Sh. Bilioni 1.8 mpaka sasa ni moja ya shule 19 za sekondari zinazojengwa Tanzania Visiwani chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Lazima (ZABEIP) miaka mitano unaogharimiwa kwa pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Dunia.
Serikali ya Mapinduzi (SMZ) inatoa dola za Marekani milioni sita na Benki ya Dunia dola za Marekani milioni 42 ikiwa ni mkopo wenye masharti nafuu na mradi wenyewe ulianza kutekelezwa Julai 2008 unafikia mwisho wake Juni mwaka huu, 2013.
Chini ya mradi huo, zinajengwa shule 10 za sekondari (kidato cha kwanza hadi cha sita) katika kila wilaya za Tanzania Visiwani, zinajengwa shule tisa za sekondari (kidato cha kwanza hadi cha nne) – tano Unguja na nne kisiwani Pemba, kinajengwa chuo kipya cha ualimu cha William Benjamin Mkapa Kisiwani Pemba na shule sita zinafanyiwa matengenezo makubwa.
Mradi huo pia ni matokeo ya mazungumzo kati ya Rais Kikwete na uongozi wa Benki ya Dunia wakati alipofanya ziara yake ya kwanza Marekani mwaka 2006 baada ya kuwa amekuwa Rais wa Tanzania ambako aliushawishi uongozi wa Benki hiyo kukubali kutoa fedha za kugharimia mradi huo mkubwa zaidi kuliko mwingine wowote kufanywa na Serikali katika historia ya Zanzibar.
Aidha, kutekelezwa kwa mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010 ambayo iliiagiza Serikali ya Mapinduzi kujenga shule za kisasa za sekondari 21 katika wilaya zote za Unguja na Pemba.
Chini ya Mradi wa ZABEIP, tayari shule za sekondari 13 zimekamilika kujengwa na ujenzi wa shule sita zilizobakia pamoja na Chuo cha Ualimu cha Benjamin William Mkapa Kisiwani Pemba unaendelea.
Na ili kufikisha idadi ya shule 21 za sekondari kama inavyoelekeza Ilani ya CCM, ujenzi wa shule nyingine mbili zilizosalia unaendelea katika eneo la Mkanyageni Kisiwani Pemba na Kiblateni Kisiwani Unguja kwa gharama ya pamoja ya Serikali ya Mapinduzi na Benki ya Kiarabu ya Maendeleo (BADEA).
Shule ya Mlimani-Matemwe yenye huduma kamili za elimu na ambayo ni sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne, ilianza kupokea wanafunzi Septemba mwaka jana kwa vidato vya kwanza na tatu. Wanafunzi 231 ndiyo walianzisha shule hiyo ya kutwa na yenye hadhi ya wilaya ikiwa na wavulana 145 na wasichana 86. Shule hiyo ina walimu tisa wakiwemo wawili wa kujitolea kutoka Nigeria.
Sherehe hizo za uzinduzi wa shule hiyo zilizohudhuriwa na viongozi wa SMZ akiwamo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Idi imehudhuriwa na mamia ya wakazi wa eneo la Mlimani-Matemwe.