Na Magreth Kinabo – Maelezo Dar es Salaam
WAKUU wa nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuia ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika (SADC TROIKA) wamekubaliana kusaidiana na umoja wa Mataifa (UN) wa kupeleka Majeshi ya Ulinzi na Usalama (NIF) katika upande wa Mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC).
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa Afrika (SADC), Tomaz Salomao wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa wakuu hao uliofanyika kwa muda wa siku mbili jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ulikuwa unajadili hali ya siasa na usalama kwa nchi za DRC, Zimbambwe na Madagascar chini ya Mwenyekiti wake (SADC TROIKA) Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete na kuhudhuriwa na Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba, Rais wa Msumbiji, Armando Emilio Guebuza, ambaye ni Mwenyekiti wa SADC na Rais wa Msumbiji, Jacob Zuma.
Akizungumzia kuhusu upande wa DRC, Salomao alisema mkutano huo umetaka misaada ya kibinadamu ipelekwe mapema iwezekanavyo katika upande wa Mashariki mwa DRC. Aliongeza kuwa wamepokea ahadi za nchi za Malawi, Namibia, Afrika Kusini na Tanzania za kuwa tayari kupeleka majeshi ya ulinzi na usalama katika upande huo, ambapo pia umezishauri nchi nyingine ambazo hazijatoa ahadi hizo kufanya hivyo haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wake Rais Kikwete akitoa ufafanuzi juu ya makubaliano ya kila nchi itachangia wanajeshi wangapi na lini zoezi hilo litafanyika alisema suala hilo bado liko kwenye mchakato na litapata majibu baadaye.
Kwa upande wa Zimbabwe Salomao alisema mkutano huo umependekeza wadau wa siasa katika nchi hiyo kuhakikisha wanaharakisha wanakamilisha utengenezaji wa Katiba mpya ili kuwezesha uchaguzi wa amani, huru, na haki.
Aliongeza kuwa katika mgogoro wa kikatiba wa nchi ya Madagascar mkutano huo umepokea maelezo, kutoka kwa Rais wa mpito wa nchi hiyo, Andry Rajoelina kuhusu mkakati wa kutatua suala hilo na kusisitiza utekelezaji wake.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Rais wa serikali ya mpito ya Madagascar Andry Rajoelina na marais wa nchi za Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini na ulioongozwa na mwenyekiti Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kutafuta suluhisho la mgogoro wa kikatiba wa Madagascar, Zimbabwe na machafuko nchini DRC.