Tucta Yataka Haki ya Migomo, Maandamano Katika Katiba

Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya



SHIRIKISHO
la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limependekeza kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, migomo na maandamano viwe haki ya msingi ya raia. Wakati Tucta likitoa pendekezo hilo, Chama cha UPDP kimeungana na CCM kutaka mgombea binafsi aruhusiwe, huku NCCR Mageuzi kikiungana na Chadema kutaka umri wa urais ushushwe na apunguziwe madaraka.

Tucta, mbali na kutaka maandamano na migomo viruhusiwe, limependekeza hayo yafanyike kisheria baada ya kufutwa sheria kandamizi zinazowabana wafanyakazi wanaodai haki na masilahi yao. Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya alisema jana baada ya kuwasilisha maoni ya shirikisho hilo kuwa Katiba Mpya lazima iwe mkombozi wa wafanyakazi.

Alisema wanataka Katiba itamke kwamba kila mfanyakazi atakuwa na haki ya kugoma na kufanya maandamano wakati wanapoona haki zao hazizingatiwi.

“Sheria zilizopo zinazoruhusu maandamano na migomo ni kandamizi. Tunataka Katiba Mpya izifute na ziwepo sheria ambazo si kandamaizi ili kuwapa nafasi wafanyakazi kudai haki zao kwa maandamano bila vikwazo.”

Mgaya alisema Katiba Mpya iwe na kifungu kitakachoeleza uhusiano kazini ili kuhakikisha wafanyakazi wananufaika na kazi wanazofanya.

“Tunataka Katiba Mpya itamke kila mfanyakazi atakuwa na haki ya kushiriki na kushirikishwa kupitia vyombo mbalimbali vya mashauriano na vinavyohusika katika uamuzi wa kazi. Hiyo itakuwa njia sahihi ya kutoa nafasi kwa wafanyakazi kueleza mambo ambayo wanaona hawanufaiki nayo katika sehemu zao za kazi,” alisema.

Pia alisema: “Tunataka Katiba Mpya itamke kwamba ndani ya Bunge kutakuwa na uwakilishi wa wafanyakazi ili kutatua matatizo ya wafanyakazi.”

UPDP na mgombea binafsi
Mkurungezi wa Sheria na Katiba wa UPDP, Juma Nassoro alisema pamoja na mambo mengine, wamependekeza mgombea binafsi aruhusiwe katika nafasi zote za uongozi isipokuwa urais. Alisema mfumo wa sasa unaolazimisha mgombea kutokana na chama cha siasa ni kuwanyima wananchi wasio na vyama kushiriki katika uongozi wa nchi kwa kutumia haki yao ya kuchagua na kuchaguliwa.

Alisema mantiki ya kutaka mgombea wa urais atokane na vyama vya siasa ni kutoa nafasi kwa wananchi kufanya tathmini za sera za vyama husika… “Yawezekana mtu akajitokeza kuwa mgombea urais na akawa na sera inayopingana na Katiba na maadili ya nchi. Ili kuepuka hilo Katiba Mpya isiruhusu mgombea binafsi kwa nafasi ya urais.”

Pia alisema wamependekeza muundo wa Serikali uwe wa Serikali tatu; Tanganyika, Zanzibar na Muungano… “Katika uongozi kwenye Serikali hizo kutakuwa na marais watatu kutoka kila Serikali huku Serikali za Tanganyika na Zanzibar zikiwa na mawaziri viongozi na ya Muungano ikiwa na waziri mkuu atakayeteuliwa na Rais wa Muungano na kuthibitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.”

CHANZO: www.mwananchi.co.tz