*Wasema gesiasilia itumike kwa manufaa ya taifa na si kwa mkoa inapotoka
WAZEE wa Tabora wameunga mkono msimamo wa miaka yote wa Serikali kwamba rasilimali za Tanzania, ikiwamo gesiasilia iliyogunduliwa katika mikoa mitatu ya Tanzania ukiwamo Mkoa wa Mtwara, itumike kwa manufaa ya nchi nzima na wala si kunufaisha mikoa ambako gesiasilia hiyo inapatikana ama imegunduliwa.
Aidha, wazee hao wameitaka Serikali kuanzisha sera na utaratibu ya kutenga sehemu maalum katika hospitali zote nchini kwa ajili ya kuhudumia wazee ambao wanapata shida kupanga foleni kwa ajili ya kupatiwa huduma za afya.
Wazee hao pia wamepongeza msimamo wa Serikali ya Rais Kikwete kuhakikisha kuwa hakuna ardhi ya Mtanzania yoyote inachukuliwa kwa matumizi ya umma bila kufidiwa na Serikali. Wazee hao walieleza msimamo wao kuhusu masuala hayo wakati walipokutana na Rais Kikwete kwa mkutano maalum uliofanyika usiku wa Januari 9, 2013, katika Ikulu Ndogo ya Tabora ambako Rais Kikwete anafanya ziara ya siku tano kukagua na kufungua miradi ya maendeleo.
Wazee hao wa CCM wa Tabora Mjini wametoa msimamo wao kuhusu gesiasilia na rasilimali nyingine nchini na kuhusu msimamo wa baadhi ya wakazi wa Mtwara ambao wamekuwa wanaendesha kampeni, isiyokuwa na tija na isiyoungwa mkono na watu, kupinga gesiasilia kusafirishwa kwenda Dar Es Salaam. Wamefanya hata maandamano kuishinikiza Serikali kubadili sera hiyo ya kihistoria ya Tanzania.
Serikali inatumia mabilioni ya fedha kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ambako itatumika kuzalisha umeme kwa wingi na kumaliza tatizo la umeme sugu la sasa nchini na pia kwa matumizi ya viwanda. Umeme utakaozalishwa kutokana na gesiasilia hiyo utaunganishwa kwenye gridi ya taifa kwa manufaa ya mikoa yote nchini. Mbali na Mtwara, gesiasilia pia imegundulika mikoa ya Pwani na Lindi ambako tayari gesiasilia yake inatumika kuzalisha umeme kwa ajili ya mikoa ya Lindi na Mtwara.
Wazee hao wamemwambia Rais Kikwete kuwa msimamo wa baadhi ya wananchi wa Mtwara, wakiongozwa na baadhi ya wanasiasa na hasa wale wa vyama vya upinzani, unashangaza kwa sababu miaka yote tokea uhuru msimamo wa Tanzania ni kwamba raslimali inayopatikana katika sehemu yoyote ya Tanzania itumike kwa ajili ya nchi nzima na watu wake na siyo kwenye mikoa inakopatikana raslimali hiyo.
“Kuhusu hili suala la msimamo wa baadhi ya wananchi wa Mtwara kuhusu gesi, tunaamini kuwa wenzatu wa Mtwara wamepotoka na kughafilika kwa sababu msimamo wetu wa kihistoria katika nchi hii ni kwamba raslimali za nchi yetu zitumike kwa ajili ya nchi nzima na wananchi wote wa Tanzania,” wamesema wazee hao katika risala yao kwa Rais Kikwete na kuongeza: “Wenzetu hawa wa Mtwara nadhani wamedandia ajenda ambayo hawaijui na hawakuianzisha wao kwa sababu kazi ya gesiasilia imefanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM) lakini wanaojaribu kuvuruga kazi hiyo ni wapinzani wa CCM.”
Rais Kikwete aliwashukuru wazee hao wa Tabora na kuwaambia kuwa kila mtu, kila mkoa ukitaka kubakia na rasilmali yake ni dhahiri kuwa haitakuwepo Tanzania. “tutaigawa nchi yetu na kuibakiza vipande vipande.”
Aliongeza Mheshimiwa Rais: “Baadhi yetu sisi wanasiasa tayari tumeharibikiwa na sasa wanatafuta namna ya kujijenga upya kwa kutumia suala la gesiasilia.”
Rais Kikwete pia alikubaliana na wazo la kuanzisha sehemu maalum ya matibabu ya wazee katika hospitali nchini. “Hili ni wazo zuri na tutaangalia jinsi gani linavyoweza kutekelezeka.”