SERIKALI, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, imetoa kwa makusudi, kandarasi ya mabilioni ya fedha kwa wakandarasi na wataalamu wengine wazalendo kwa nia ya kuunga mkono wanataaluma Watanzania na kuwapa nafasi kubwa zaidi katika kuchangia maendeleo ya nchi yao.
Kandarasi hiyo ni ujenzi wa Daraja la Mto Mbutu, Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora daraja ambalo ujenzi wake utawanufaisha maelfu ya wananchi katika wilaya hiyo na wilaya za jirani za Iramba (Mkoa wa Singida), Meatu (Mkoa wa Simiyu) na Kishapu (Mkoa wa Shinyanga).
Kandarasi hiyo ina thamani ya Sh. Bilioni 11. 286 ya kazi ya usimamizi, ushauri na ujenzi wa daraja hilo utakuwa moja kwa moja kwa asilimia 100 mikononi mwa wataalamu Watanzania ambao wamekusanya nguvu zao kuweza kushinda kandarasi hiyo.
Undani wa kandarasi hiyo ulitangazwa juzi, Jumapili, Januari 6, 2013, wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alipoweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Daraja hilo ambalo wataalam hao wazalendo wameahidi kuwa ujenzi wake utakamilika ifikapo Novemba, mwaka huu, 2013.
Miongoni mwa wataalamu hao wazalendo waliopewa kandarasi hiyo ni pamoja na makampuni 13 ya makandarasi, makampuni ya washauri na makampuni ya wasimamizi.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli alimwambia Rais Kikwete kuwa kandarasi hiyo imetolewa kwa wataalam wazalendo kulingana na ahadi ambayo Rais aliitoa wakati alipozungumza na wataalamu hao wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya kuundwa kwa vyama vya kitaalamu vya sekta ya ujenzi mwaka juzi 2011.
“Mheshimiwa Rais, uliahidi kuunga mkono makandarasi wazalendo na kazi hii umeifanya. Tuna wakandarasi waliosajiliwa kiasi cha 9,447 kwa sasa nchini. Zamani walikuwa wanapata asilimia 30 ya miradi yote ya ujenzi nchini. Chini ya uongozi wako, sasa asilimia hiyo imepanda katika miaka ya uongozi wako hadi kufikia asilimia 50. Na sasa umetoa kandarasi hii. Tunakushuru sana.”
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Makandarasi nchini, Mhandisi Consolata Ngimbwa alimwambia Rais Kikwete katika sherehe hizo za uwekaji jiwe la msingi: “Haijawahi kutokea. Katika historia ya Tanzania, hakuna Rais aliyewahi kuwaamini watalaam wa nyumbani kwa kutoa kandarasi kubwa kiasi hiki kwa makandarasi wa nyumbani ama wataalam wengine wa Kitanzania. Tunakushukuru sana, sana Mheshimiwa Rais.”
Naye Rais Kikwete alisema: “Niliahidi kuwa Serikali ingewapa kazi, tena kazi kubwa. Lakini wakati huo niliwaambia kuwa kikwazo cha kupata kazi kubwa kilikuwa ni udogo wenu, kila mtu na lwake. Niliwaambia kuwa katika mambo haya kupiga uzalendo peke yake lilikuwa ni jambo halitoshi. Niliwaambia kuwa nguvu ya mnyonge ni umoja, Nashukuru kuwa mmelitambua hili na kujiunga katika umoja wenu. Dumisheni umoja huu.”
Aliongeza: “ Hii kazi tuliyowapa ni majaribio. Mkiweza kuifanya kazi hii vizuri basi utakuwa ni ufunguo wa kupata kazi nyingine. Hii ni flagship yenu.”