Dkt Shein Afungua Mitambo ya Dijitali na Jengo la Mawasiliano Unguja

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akikata utepe kufungua jengo la Mradi
wa Kuhama kutoka Teknolojia ya Analojia kwenda Digital hapo Rahaleo
Mjini Zanzibar,ikiwa ni shamra shamra za kuaadhimisha miaka 49 ya
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. [Picha na Ramadhan Othman,IKulu.]

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa hatokuwa tayari kuona serikali anayoiongoza iko nyuma katika tasnia ya habari na mawasiliano.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Rahaleo, Mjini Unguja, mara baada ya kufungua mitambo ya Dijitali na jengo la studio ya kurekodia muziki ambalo limefanyiwa ukarabati mkubwa.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuhakikisha sekta hiyo ya habari na mawasiliano Zanzibar inaimarika na kurejea katika uwasilia wake.
Alisema kuwa Zanzibar ina historia kubwa katika setka hizo hivyo aliutaka uongozi na wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji la Zanzibar kubadilika na kutofanya kazi kwa mazoea’busnes is ussual’.
Dk. Shein alisema kuwa juhudi kubwa zinachukuliwa na serikali ikiwa ni pamoja na kuekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu hiyo ya digitali pamoja na kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la studio na kurekodia muziki, hivyo kuwataka watendaji kufanya kazi kama wanavyofanya wenzao katika vyombo vya habari.
Alisema kuwa umefika wakati kwa watendaji wa Wizara hiyo kuleta mabadiliko katika utendaji wao wa kazi vyenginevyo wataachwa nyuma.
Dk. Shein alisisitiza kuwa wananchi wengi wa Zanzibar bado hawajaridhika na wamekuwa wakinungunika juu ya ufanyaji kazi wa televisheni na redio ndani ya Shirika la Utangazaji ka Zanzibar (ZBC).
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa chimbuko la sinema pamoja na michezo ya kuigiza Zanzibar linatokana na jengo hilo na kusisitiza haja ya kufanyiwa kazi iliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuzirekodi kazi za wasanii.
Alieleza kuwa kuna kazi nyingi za wasanii ambao wengine tayari wameshafariki na wengine bado wako hai, ambapo kazi zao ni nzuri na kuna haja ya kufanyiwa kazi huku akisisitiza kuwa kwa wasanii waliokufa ni vizuri kupata ruhusa kutoka kwa familia zao pale wanapohitaji kupiga ama kuonesha sanaa zao.
Alieleza kuwa hiyo ni kutokana na kuwa wapo wanaofurahia kusikia kazi hizo na wapo ambao hawapendezewi kusikia ndugu ama jamaa zao waliofariki wakiimba ama kuonesha sanaa zao katika vyombo vya habari.
Alisisitiza kuwa kwa kuona uimarishwaji wa sanaa pamoja na kuwepo wka vipaji lukuki hapa Zanzibar ndio alipata mori na kuahidi kuwapatia vijana hao wa sanaa mahala pakuweza kurekodi kazi zao za muziki na kufanya maonesho ya sanaa zao.
“Jengo hili lilikuwa likiitwa Sauti ya Unguja na bnaadae likaitwa Sauti ya Tanzania Zanzibar na nilipopita katika ziara yangu ndipo nikaagiza lirejeshwe katika shughuli zake za asili”,alisema Dk. Shein. Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuimarishwa michezo, utamaduni pamoja na mashindano ya riadhaa hapa nchini.
Pia, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Kampuni ya Agape ambayo ndio inayoshughulikia mradi huo wa digitali hapa Zanzibar kwa utendaji wao wa kazi huku akisisitiza kuwa Zanzibar itaingia kwenye mfumo huo februari 28 mwaka huu ikiwa na uhakika zaidi wa mfumo huo baada ya kuunganishwa na mtandao wa e-government kwa ajili ya kuona mambo zaidi duniani.
Alisema kuwa mitambo hiyo itakwenda na wakati na haitobadilika hata kukitokea mabadiliko mengine duniani kama yalivyotokea hivi sasa.
Nae Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk alieleza kuwa mitambo ya dijitali iliyoizundua Rais ni ya uhakika ambayo inatoka Marekani na Ujenrumani na kusema kuwa vingamuzi vitakavyotolewa na ZBC havitozidi shilingi 50elfu na kwa mwezi malipo hayatozidi elfu8 ambapo chanal zake zitakuwa 36 hadi 38.
Alisema kuwa ZBC itahakikisha vijana, wazee na watoto wanafaidika na chanal zitakazokuwemo katika vingamuzi hivyo ambavyo vitatolewa katika Wilaya zote 10 za Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akipata maelezo ya matumizi ya vifaa
vya Dijital,kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Agape Association
LTD,Dr Vernon Fernandes,(kulia) baada ya kufanya uzinduzi wa Mradi wa
Kuhama kutoka Teknolojia ya Analojia kwenda Dijital hapo Rahaleo Mjini
Zanzibar,ikiwa ni shamra shamra za kuaadhimisha miaka 49 ya Mapinduzi
Matukufu ya Zanzibar,(kushoto) Dk.Anny Fernandes, [Picha na Ramadhan
Othman,IKulu.]

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ali Mwinyikai, alisema aliwataka wananchi kuwa na subira kwani jambo kubwa lililochelewesha Zanzibar kuingia kwenye Digitali ni kutaka kuingia katika mfumo huo kwa uhakika zaidi ikiwa ni pamoja na kuwa na vingamuzi vilivyobora baada ya kufanya utafiti mkubwa.
Alisema kuwa ujenzi wa miundombinu ya Dijitali umegharimu zaidi ya Bilioni 8 ambapo matengenezo ya jengo hilo lililofanyiwa ukarabati mkubwa yamegharimu shilingi milioni 195 za Kitanzania.