RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Jumatatu, Januari 7, 2013, ameweka jiwe na msingi kwenye ujenzi wa daraja kubwa na kuzindua mradi mkubwa wa maji katika Mkoa wa Tabora ambako anafanya ziara ya kikazi ya siku nne kukagua, kuweka jiwe la msingi na kuzindua miradi ya maendeleo.
Katika tukio ambalo ni la kihistoria tokea Tanzania kupata uhuru, Rais Kikwete ameanzisha rasmi ujenzi wa daraja kwenye Mto Mbutu, nje kidogo tu ya mji wa Igunga, kwa kuweka jiwe la msingi la daraja ambalo litatoa huduma kwa wakazi wa mikoa ya Tabora, Singida, Shinyanga na Simiyu.
Wakati Rais akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Daraja hilo katika sherehe ya kufana iliyohudhuriwa na maelfu ya wananchi wa mji wa Igunga na vijiji vya jirani, wananchi waliendelea kuvuka Mto huo uliojaa maji kutokana na mvua zinazoendelea sasa Mkoani Tabora kwa kutumia miguu wengi wakiwa wamebeba baiskeli, pikipiki, mifugo na mali zao nyingine vichwani mwao kuelekea mjini Igunga kwenye masoko.
Ujenzi wa Daraja la Mbutu ni utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na ahadi ya Mheshimiwa Rais Kikwete wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huo ambako aliahidi kuwa Serikali yake ingejenga daraja kwenye Mto huo ambao huhamahama kutegemea wingi wa maji.
Daraja hilo litawanufaisha moja kwa moja wakazi 84,000 wa kata saba za Mkoa wa Tabora na wakazi wa wilaya jirani za Iramba (Mkoa wa Singida), Meatu (Mkoa wa Simiyu) na Kishapu (Mkoa wa Shinyanga) na mzungumzaji mmoja baada ya mwingine katika sherehe hizo ameelezea ujenzi wa daraja hilo kuwa ni ukombozi mkubwa wa wananchi wa eneo hilo. Inakadiriwa kuwa ujenzi wa daraja hilo utakamilika Novemba mwaka huu na utagharimu kiasi cha Sh. bilioni 11.286 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.
Rais Kikwete pia amezindua Mradi wa Maji na Chujio la Maji la Mji wa Igunga katika kijiji cha Bulenya, nje kidogo ya Mji huo wa Igunga.
Mradi huo uliogharimu kiasi cha Sh. Bilioni 6.7 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania utawanufaisha wakazi wa Mji wa Igunga na vijiji vitatu vinavyozunguka mji huo ambao wakazi wake sasa wataweza kupata maji kwa asilimia 70.
Kiasi cha watu 32,600 watanufaika na maji ya mradi huo ambao sasa watakuwa wanapata lita 2,600 za maji kwa siku badala ya lita 710 za sasa.