Na James Gashegu, EANA
Arusha, Januari 5, 2013 (EANA) – Mwaka uliomalizika wa 2012 imeshuhudia ucheleweshwaji wa aina yake katika mipango ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikiwa ni pamoja na kusogezwa mbele kuanzishwa kwa Umoja wa Fedha ambao sasa unatarajiwa Novemba mwaka huu.
Yafuatayo ni matukio mengine muhimu kwa EAC kwa mwaka uliopita kama yalivyofuatiliwa na Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki(EANA)
EAC yapata ofisi zake za kudumu
Mwaka 2012 utaendelea kukumbukwa katika historia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwa ni mwaka ambao taasisi hiyo ya kanda ilihamia katika ofisi zake za kudumu baada ya miaka mingi ya kukodi ofisi ghali za Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Arusha (AICC).
Makao makuu ya EAC yana ofisi zake sasa zenye eneo la mita za mraba 15,025 na majengo matatu yenye ghorofa nne kila moja.
Ujenzi wa ofisi hizo ulizinduliwa na wakuu wa nchi tano zinazounda jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi Novemba 20, 2009, ingawaje ujenzi rasmi ulianza Januari 28, 2010.
Mradi huo umefadhili wote kwa ujumla wake na Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kwa gharama ya Euro 14.8 milioni.
Margret Zziwa Nantongo achaguliwa Spika wa bunge la EAC
Margret Zziwa Nantongo alichaguliwa na wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kuwa Spika wa Bunge hilo baada ya kumshinda mganda mwenzake,Dora Byamukama.
Spika huyo mpya ambaye aliapishwa na Katibu wa Bunge hilo, Kenneth Madete mara baada ya uchaguzi huo alinyakua ushindi wa kura 33 katka raundi ya pili ya upigaji kura.
Byamukama kwa upande wake aliambulia kura 12 ikiwa ni chini kutoka kura 18 alizopata katika raundi ya kwanza.
Mbuge huyo wa EALA amechukua nafasi ya uspika iliyoachwa wazi na Mkenya, Abdulaihin Abdi aliyeshikilia nafasi hiyo kwa miaka mitano, akirithi kutoka kwa mtanzania, Abdurahman Kinana.
Katika kikao cha kwanza cha Bunge la tatu kilichokaa Nairobi,Kenya Zziwa alikiri kwamba licha ya utekelezaji wa mihimili ya awali ya mtangamano- Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja, changamoto nyingi za utekelezaji wa mtangamano mzima bado zinaendelea kuwapo. Miongoni mwa changamoto alizozitaja ni pamoja na vikwazo vinavyokwamisha utendaji wa biashara ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa vizuizi visivyo na kodi na ugoigoi wa agenda mpya katika sera za kitaifa kuhusu EAC.
Mabunge ya kitaifa yakubali kuanzisha kamati za kushughulikia masuala ya mtangamano
Katika mkutano wa Maspika wa Mabunge ya Afrika Mashariki mjini Kigali, Rwanda Mei 2012,mabunge yote ya kitaifa katika kanda hiyo yamekubaliana kuanzisha kamati maalum kushughulikia masuala yanayohusu mtangamano wa kikanda na kutenga muda maalum ili kujadili masuala hayo kama ilivyo katika kamati zilizopo katika mabunge ya kitaifa.
Barabara ya Arusha-Namanga-Athi River iliyokarabatiwa yazinduliwa rasmi
Wakuu wa nchi za EAC Novemba 2012 walizindua rasmi barabara ya Arusha-Namanga-Athi River iliyofanyiwa ukarabati mkubwa. Uzinduzi huo ulifanyika Athi River, nchini Kenya.
Maombi ya Sudani Kusini, Somalia kujiunga EAC yasogezwa mbele
Matarajio ya Sudani Kusini na Somalia kujiunga na EAC yamesogezwa mbele baada ya wakuu wa nchi za EAC kwa mara ya pili kuongeza muda wa kufanya maamuzi juu ya maombi ya nchi hizo mbili kujiunga na jumuiya hiyo.
Katika mkutano wao mjini Nairobi, wakuu wa nchi za EAC waliuagiza Mkutano wa Baraza la Mawaziri kufanya majadiliano zaidi na nchi huru mpya ya Sudani Kusini ambapo pia kuzingatia katika mammbo yaliyopatikana katika ripoti ya kamati kuhusu Somali.
Hii ni mara ya pili kwa maombi ya nchi hizo mbili kusogezwa mbele, la kwanza likiwa la Aprili 2012 katika mkutano wa wakuu wa nchi wanachama mjini Bujubura, Burundi.
Katika mkutano wa mjini Nairobi pia wa wakuu wa nchi wanachama, Marais walipitisha itifaki mbalimbali ikiwa ni pamoja na ya Amani na Usalama na ile ya Habari, mawasiliano na mtandao wa teknolojia.
Kurahisisha usafirishaji bidhaa
Kwa kipindi cha mwaka jana, kanda hii pia ilishuhudia kuanzishwa kwa Mradi wa Uangalizi wa Usafirishaji ili kusimamia malori makubwa yanayosafirisha bidhaa ndani ya kanda kwa kutumia vifaa vya kielektroniki kubaini sababu za ucheleweshwaji katika njia zinazopitia.
Mpango huo uliozinduliwa mjini Mombasa, Kenya unafadhiliwa na kampuni ya TradeMark East Afica (TMEA) na kuasisiwa na Transit Transport Coordination Authority of the Northern Corridor (TTCA) na Chama cha Wasafirishaji cha Kenya.
Katika mradi huo, malori makubwa huwekwa vifaa vya kutambua mahali lilipo katika safari yake (GPS) na ambacho kinarekodi kila mahali linaposimama katika safari yake.Pamoja na kupewa kifaa hicho,madereva pia hupewa fomu za kujaza kwa nini wamesimamishwa wakiwa safarini.
Mwaka uliopita EAC imeshuhudia pia Rwanda kupitia Wazara yake inayoshughulikia masuala ya mtangamano ikizindua sera yake ya kitaifa juu ya mwendendo wa mtangamano wa EAC ili kufuatilia maslahi yake katika jumuiya hiyo.
Sera hiyo mpya inalenga katika maeneo matano muhimu ikiwa ni pamoja na kuingiza mtangamano wa kikanda katika maendeleo ya Rwanda, kuhusisha taasisi za EAC,kupunguza na kulinda hatua zitakazolenga kupunguza athiri hasi kwa Rwanda katika mwenendo mzima wa mtangamano.
Sera hiyo pia inaangalia maeneo mengine ya kufanya maamuzi katika EAC na majukumu yake na mfumo wa kitaasisi utakaoratibu, kusimamia na kutathmini utekelezaji wa mipango ya EAC nchini Rwanda.
Rwanda inakua nchi ya kwanza katika jumuiya hiyo kuweka mkakati wa aina hii miongoni mwa nchi tano za EAC.
Waziri wa Masuala ya EAC wa Rwanda, Munique Mukaruliza alieleza kwamba kanda hiyo inaendelea kukabiliana na changamoto za utekelezaji,hivyo kulazimika kuanzisha juhudi kama hizo ili kuikabili hali hiyo.
Jessica Eriyo awa Naibu Katibu Mkuu mpya wa EAC
Naibu Katibu Mkuu huyo, anamrithi Beatrice Kiraso, aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo akishughulikia Shirikisho la Kisiasa na ambaye mhula wake wa pili wa kazi ulikuwa umemalizika
Uteuzi wa Eriyo ulithibitishwa katika kikao maalum cha 10 cha wakuu wa nchi za EAC kilichofanyika Arusha,Tanzania Aprili 28, 2012.
Katika kikao hicho pia, mkataba wa kazi wa Naibu Katibu Mkuu, Jean Claude Nsengiyumva aliyekuwa anashguhuikia Tija na Sekta ya Kijamii uliongezwa.
Mabalozi vijana wa EAC
Ni mwaka huo wa 2012 ambapo EAC kwa kupitia uungwaji mkono na Kituo cha EAC cha Utafiti wa Amani cha Nyerere(NCPR) na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) walijitokeza na wazo la kuanzisha Mabalozi wa vijana wa EAC.
Mabalozi Watano wa Vijana wa EAC (kutoka kila nchi mwanachama) waliteuliwa baada ya kuibuka washindi bora kabisa katika mashindano ya kwanza wa Mdahalo wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu EAC juu ya Mtangamano wa Kanda.
Museveni achukua nafasi ya Uenyekiti wa EAC
Rais Yoweri Museveni wa Uganda Desemba alichukua nafasi ya kuwa mwenyekiti wa taasisi hiyo ya kanda ya EAC katika kipindi cha mwaka mmoja ujao katika kikao cha kawaida cha 14 cha wakuu wa nchi wananachama EAC kilichofanyika mjini Nairobi, Kenya.
Mkutano huo uliofanyika katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Kenyatta pia ulishuhudia kutiwa saini kwa barua yenye lengo la kukuza biashara baina ya EAC na Marekani.
Rais Museveni alimpongeza Rais Mwai Kibaki wa Kenya kwa kuliongoza jahazi la EAC kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Kwa upande wake, Rais Kibaki alisema miongoni mwa mafanikio ya EAC ni pamoja na uanzishwaji wa Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja.