JK Ashuhudia uwekwaji wa Wakfu KKKT Singida

Rais Jakaya Akisalimiana na Askofu Malasusa

Dkt Jakaya Mrisho Kikwete Januari 6, 2013, ameungana na mamia ya waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kushuhudia uwekwaji wakfu na kusimikwa kwa Askofu Mteuli Dkt. Alex Seif Mkumbo kuwa Askofu mpya wa Dayosisi ya Kati ya Kanisa hilo.
Katika sherehe kubwa iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Imanuel mjini Singida, Rais Kikwete pia ameshuhudia kusimikwa kwa Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mchungaji Syprian Yohanna Hilinti.
Rais Kikwete ambaye aliwasili mjini Singida j, Jumamosi, Januari 5, 2012 kwa ziara ya siku mbili za kikazi katika Mkoa wa Singida, amewasili kwenye Kanisa hilo kiasi cha saa nne unusu asubuhi na kupokelewa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Mkuu Dkt. Alex Gehaz Malasusa na mamia kwa mamia ya waumini waliohudhuria ibada na sherehe za kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu.
Askofu Mkumbo na Mchungaji Hilinti wanachukua nafasi za Askofu Eliuphoo Yohana Sima na Mchungaji Yohana Ramadhani Mujungu na walichaguliwa kushika nafasi hizo katika Mkutano wa Uchaguzi (SINODI ya 12) wa KKKT Dayosisi ya Kati uliofanyika katika Usharika wa Kanisa Kuu Imanuel, Singida, Juni 27 hadi 29 mwaka jana, 2012.
Katika sherehe zilizofanyika jana na kuhudhuriwa pia na viongozi wa Serikali na wageni kutoka nje ya nchi, Askofu Mkumbo amepitishwa katika hatua mbili ili kukamilisha nafasi yake kama Askofu wa Jimbo la Kati na Mkuu wa KKKT katika Dayosisi hiyo.
Katika hatua ya kwanza, Askofu Mteule Mkumbo aliwekwa wakfu wa kuwa Askofu wa Dayosisi ya Kati ya KKKT katika shughuli iliyosimamiwa na Askofu Dkt. Martin Fuataeli Shao, Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini akisaidiwa na Askofu Charles Robson Mjema, Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Pare na Askofu Dkt. Hans-Jurgen Abromeit, Mkuu, Pomeranian Evangelical Church (Lutheran Church in Northern Germany).
Kwa nafasi yake hiyo, Askofu Mkumbo anakuwa mwangalizi wa shughuli zote za Dayosisi pamoja na maisha ya kiroho katika Dayosisi. Aidha, anakuwa msimamizi wa huduma ya kichungaji na maisha ya familia ya kiuchungaji.
Katika hatua ya pili, Askofu Mkumbo amesimikwa kuwa Mkuu wa KKKT katika Dayosisi ya Kati shughuli ambayo imefanywa na Mkuu wa Kanisa KKKT Askofu Mkuu Dkt. Malasusa. Nafasi hii inampa Askofu madaraka kamili ya utawala na uendeshaji wa Dayosisi na kuwa wakili mwema wa mali zote za Dayosisi
Baada ya shuguli za kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Mkumbo, naye katika nafasi yake mpya amemsimika Msaidizi wa Askofu, Mchungaji Syprian Yohana Hilinti.