Askari Aliyepiga Picha na Lema Akamatwa

Abubakari Sufiani (29)

HATIMAYE mtu anayedaiwa kuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Abubakari Sufiani (29), ambaye alipiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kwenye mkutano wa Chadema uliofanyika katika Mji Mdogo wa Mirerani, Simanjiro Mkoa wa Manyara amekamatwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa alisema Sufiani alikamatwa jana katika eneo la Boma Ng’ombe, wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro kwa ushirikiano wa polisi na askari wa JWTZ baada ya kumsaka kwa wiki mbili sasa.

Desemba 23, mwaka jana katika mkutano uliofanyika Mirerani, ikiwa ni siku chache tangu Mahakama ya Rufani kumrejeshea Lema ubunge, Sufiani huku akiwa amevalia sare za JWTZ alipiga picha na Lema pamoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari huku akionyesha ishara ya vidole viwili inayotumiwa zaidi na chama hicho.

Baada ya tukio hilo la kupiga picha, Sufiani alikaririwa na gazeti hili akisema yupo tayari ikibidi, kufukuzwa jeshini, lakini siyo kuacha kushabikia Chadema akiamini kuwa ni chama makini chenye uwezo wa kuongoza nchi kwa kuwa kinatetea wanyonge na kujali masilahi ya jamii.

Kamanda Mpwapwa alidai kuwa mtu huyo siyo mwanajeshi kwani alijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kambi ya Makutupora, mkoani Dodoma mwaka 2003 na mwaka uliofuata alijiunga na mafunzo ya JKT Kambi ya Kabuku, mkoani Tanga lakini baada ya siku kadhaa alitoroka na kuanza utapeli mitaani akijidai yeye ni askari wa JWTZ.
“Hivi sasa suala hilo la Sufiani limeshatoka mikononi mwetu na linashughulikiwa na polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro kwani huko ndipo mtuhumiwa huyo alipokamatiwa,” alisema Kamanda Mpwapwa.

Alisema Sufiani alihojiwa Kituo cha Polisi Mirerani na alitarajiwa kurudishwa Boma Ng’ombe. Wengine waliohojiwa ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Endiamtu, Edmund Tibiita na mwenye nyumba aliyokuwa amepanga kijana huyo, Salvatory Simon.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema jana kwamba Sufiani anaendelea kuhojiwa kuhusiana na kitendo hicho cha kudaiwa kuvaa sare za JWTZ na kujifanya kuwa ni askari wa jeshi hilo.

Hata hivyo, mmoja kati ya askari polisi walioshiriki kumkamata mtu huyo alidai kuwa katika mahojiano na polisi yaliyofanyika Mirerani na Boma Ng’ombe, Sufiani alikana kuvaa sare hizo za jeshi.

“Sufiani alisema yeye hajawahi kuvaa sare za jeshi hilo na hata katika mkutano wa Chadema hajawahi kufika akiwa na sare hizo za JWTZ amekataa katakata,” alisema askari huyo ambaye aliomba jina lake lisiandikwe kwa kuwa siyo msemaji. Katika maelezo yake Tibiita alidai kuwa Sufiani aliwahi kufika ofisini kwake akiwa na sare hizo za JWTZ .na kudai ni mlinzi wa eneo la Mizinga.

Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe alisema wamepata taarifa za Polisi kuhusu kukamatwa mtu aliyejifanya mwanajeshi aliyepiga picha na Lema. “Baada ya kupata taarifa hizo, Jeshi limetuma ujumbe kwenda Arusha ili kupata maelezo ya kina kuhusu mtu huyo,” alisema Mgawe.
Alisema baada ya kupata maelezo hayo, jeshi litatoa taarifa kuhusiana na suala hilo.

http://www.mwananchi.co.tz