Dk Shein Atoa Salamu za Mwaka Mpya 2013

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Dk Ali Mohamed Shein,akitoa salamu za kuukaribisha Mwaka mpya wa 2013, kwa wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote, pia aliwasihi wananchi kuendela kushirikiana na Serikali yao katika kuendeleza mipando mbali mbali ya maendeleo na kuwataka kuwa walinzi wa rasilimali pia kuzingatia taratibu za kisheria, kwa kuwa na elimu bora ya rasilimali hizo. [Picha na Ramadhan Othman, Ikulu]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia wananchi kuwa neema, baraka na mafanikio zaidi yatapatikana nchini iwapo watashikamana na kusimamia amani na utulivu pamoja na kufanya shughuli halali za kujitafutia vipato.

Dk. Shein aliyasema hayo Ikulu mjini Zanzibar, katika salamu za kuukaribisha mwaka mpya wa 2013 alizozitoa kwa wananchi kupitia katika vyombo vya habari. Katika salamu hizo Dk. Shein alisema kuwa tayari neema ya kuwepo vyakula mbalimbali, kuimarika kwa biashara na shughuli nyengine za kijamii, mambo ambayo jamii nyengine wanayakosa katika kipindi cha kumaliza mwaka.

Alieleza kufarajika kwake kwa hatua kubwa za maendeleo ambayo Zanzibar imefikia ndani ya kipindi cha mwaka mmoja unaomalizika katika sekta mbalimbali za maendeleo, kiuchumi, kijamii na uimarishaji wa miundombinu na huduma za jamii. Dk. Shein alisema kuwa kumekuwa na mafanikio ya kuridhisha katika kuimarika kwa huduma za jamii zikiwemo huduma za afya, elimu, upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na upatikanaji wa chakula cha kutosha kutokana na juhudi za wakuliwa na wafanyabiashara.

Alisema kuwa ukuaji wa maendeleo katika nchi yoyote hutegemea sana kuimarika kwa hali ya amani na utulivu katika nchi. Dk. Shein alieleza kuwa pamoja na kuimarika kwa hali ya amani na utulivu nchini katika nyakati mbali mbali kwenye mwaka unaomalizika lakini vyombo vya ulinzi na usalama vimeweza kuidhibiti hali hiyo na hivi sasa inaendelea vizuri.

Kwa mara nyengine tena Dk. Shein alitoa pole kwa wananchi wote walioathirika kwa namna mbali mbali kutokana na vitendo vya ghasia na uvunjaji wa amani vilivyosababisha hasara kubwa na usumbufu kwa wananchi.

“Navipongeza vikosi vyetu vyote vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri walioifanya katika kuimarisha hali ya amani na utulivu nchini,” alisisitiza Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein aliwanasihi wananchi wote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuzuia vitendo vyovyote vya uvunjaji wa sheria kwa kuelewa kuwa huo ni wajibu wa raia wema na kufanya hivyo kutachangia kuwepo kwa hali ya amani, utulivu na mshikamano. Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar imeendelea kujijengea taswira njema kwa marafiki na taasisi mbali mbali za Kimataifa kutokana na mafanikio yaliopatikana baada ya kuanzishwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa.

Kutokana na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa ni vyema mafanikio hayo yakazidi kuendelezwa kwa faida ya kila mmoja na kuzidi kuaminiana pamoja na kuongeza umoja na ushirikiano kwa kila siku zinazvyokwenda mbele.
Dk. Shein aliwasihi wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali yao katika utekelezaji wa mipango mbali mbali ya maendeleo pamoja na kuzitumia fursa zilizopo za kujiletea maendeleo.

Katika salamu hizo, Dk. Shein aliwakumbusha wananchi wajibu wao wa kulinda miundombinu mbali mbali iliyojengwa kwa gharama kubwa zikiwemo barabara, nguzo za umeme, waya, pamoja na sehemu zilizopitia mtandao wa Serikali (e-Government). Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka wananchi wote kuwa walinzi wa rasilimali ziliopo na kuhimizana kuzingatia sheria katika matumizi bora ya rasilimali hizo kwa faida yao na vizazi vijavyo.

Dk. Shein aliwatakia wananchi wote kheri ya mwaka mpya wenye mafanikio na baraka huku akitoa nasaha zake kwa kila mmoja kutia nia ya kuongeza ufanisi katika utejkelezaji wa shughuli zake popote alipo.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwatanabahisha wananchi kuwa katika kusherehekea mwaka mpya kuzingatia maadili yao na taratibu za kisheria zilizopo. “ Nawasihi watu wote washerehekee mwaka mpya kwa amani, mapenzi baina yetu na umoja na haya yawe malengo yetu makuu kwa ajili ya maendeleo yetu,” alisisitiza Dk. Shein.