MICHUANO YA KOMBE LA KAGAME

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekubali kuwa mwenyeji wa
mashindano ya Kombe la Kagame yanayoshirikisha klabu bingwa za nchi wanachama wa
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Klabu 12 zitashiriki katika mashindano hayo yatakayofanyika nchini kuanzia Juni
25 hadi Julai 9 mwaka huu.

Tumechukua uamuzi huu mgumu wa kuandaa mashindano haya kwa lengo la kuyaokoa.
Awali mashindano hayo ambayo yalianzia nchini mwaka 1974 yalikuwa yafanyike
Zanzibar ambayo ilijitoa.

Baadaye yalihamishiwa Sudan ambapo napo yalikwama baada ya Serikali ya nchi hiyo
kutokuwa tayari kuwa mwenyeji kwa sasa kutokana na sababu mbalimbali.

Hivyo tunaziomba kampuni mbalimbali nchini zijitokeze kwa ajili ya udhamini
ambao utawezesha kufanyika kwa ufanisi.

Jumatatu (Juni 20 mwaka huu) tutakuwa na mkutano na waandishi wa habari kuelezea
taratibu za mashindano hayo ikiwemo timu zitakazoshiriki. Tanzania kwa kuwa
mwenyeji itaingiza timu mbili.

Boniface Wambura
Ofisa Habari