WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amezindua mradi wa umeme jua (solarpower) wenye thamani ya sh. milioni 910 kwa ajili ya shule za sekondari na zahanati katika jimbo la Katavi ambao unagharimiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo.
Akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mpanda, Bw. Estomih Chang’a alisema mradi huo ambao unatekelezwa kwa awamu tatu, unagharimiwa na Serikali kwa kushirikiana na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Alisema katika awamu ya kwanza, mradi huo ulioanza Januari 15, 2012 hadi Aprili 27, 2012, uligharimu sh. milioni 139,718,375/-. “Jumla ya madarasa nane, mabweni manne, nyumba za walimu nane, zahanati moja na kituo cha afya kimoja vilinufaika na mradi huo,” alisema Bw. Chang’ah katika uzinduzi uliofanyika mwishoni mwa wiki kwenye shule ya sekondari ya Usevya kata ya Usevya ukiwakilisha shule zote za sekondari katika jimbo.
Katika awamu ya pili, mradi huo uligharimu sh. milioni 156,831,432 kwa kuweka umeme kwenye madarasa 16, mabweni mawili, zahanati mbili na nyumba za walimu saba na jengo la utawala kwenye shule moja ya sekondari.
Alisema awamu ya tatu ambayo imeanza hivi sasa na inatarajiwa kukamilika ifikapo Februari 20, 2013, inatarajiwa kugharimu sh. milioni 492,451,000/- kwa kuweka umeme kwenye madarasa 15, mabweni manne, bwalo moja la chakula na nyumba za walimu tano.
“Maeneo mengine yatakayohusika ni zahanati nane, majengo ya utawala kwenye shule nne za sekondari, nyumba nane za watumishi, nyumba na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nsimbo, nyumba na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlele pamoja na nyumba na ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Mlele,” alisema.
Akizungumza na wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita pamoja na walimu wa sekondari ya Usevya, Waziri Mkuu alisema kabla ya kuanza kwa mradi alikuwa amepata ufadhili kutoka Japan kwa ajili ya shule tu na tatizo likawa ni namna ya kugawa huduma hiyo kwa jimbo zima.
“Nilipeleka wazo hili katika kamati ya kusimamia mfuko wa fedha za jimbo ndipo tukakubaliana kuwa tuwashe umeme katika shule zote za sekondari, zahanati zote na vituo vya afya. Tulikubaliana kuwa mwaka hadi mwaka tutachukua fedha yote na kuingiza katika mradi huu ili kuleta chachu ya maendeleo kwa wananchi,” alisema.
Alisema waliamua kulenga shule na zahanati kwa kuwa walimu wanahitaji kuandaa masomo na kusahisha kazi za wanafunzi, wanafunzi wanahitaji kujisomea jioni, na kwenye zahanati waliamua hivyo kwa sababu ugonjwa hauchagui saa ya kumpata mtu.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Katavi alisema mwakani anatarajia kuanza kuweka umeme kwenye shule za msingi hasa katika nyumba za walimu na katika madarasa angalau mawili ili wakati wa jioni wanafunzi waweze kupata fursa ya kujisomea au kupata masomo ya ziada kutoka kwa walimu wao.