Waziri Pinda Atangaza Amri 10 za Kuendeleza Kilimo

Mahindi shambani

Na Mwandishi Maalumu, Katavi

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amefanya ziara ya ghafla kwa kukagua mashamba ya viongozi wa mkoa wa Katavi kwa kuanza na shamba la Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Rajab Rutengwe. Pia alikagua shamba la na Katibu Tawala wa Mkoa, Mhandisi Emmanuel Kalobelo. Mashamba yote mawili yako katika kijiji cha Songambele eneo la tankifupi, kata ya Nsimbo, wilayani Mlele, mkoani Katavi.

Shamba la Mkuu wa Mkoa lenye ukubwa wa ekari tano lilikuwa limepandwa mahindi na linatumika kama shamba darasa wakati lile la Katibu Tawala wa Mkoa lenye ukubwa wa ekari nne na nusu lilikuwa limepandwa mahindi na miembe ya kisasa. Pia kulikuwa na banda la ng’ombe.

Waziri Mkuu alichukua uamuzi huo Desemba 17, 2012 mara baada ya kuzungumza na wakazi wa kijiji cha Songambele kwenye kata ya Nsimbo na kuwatangazia amri 10 za kuendeleza mkoa huo na wilaya yao mpya.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya tano ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi alisema amelazimika kuandaa amri hizo 10 kwa sababu anatambua kwamba kila mtu anahitaji kula chakula bila kujali kama mtu huyo ni kiongozi wa ngazi ya juu, mwananchi wa kawaida au ni kiongozi wa dini.

“Tumbo halijali wewe ni Waziri Mkuu, mwalimu, Mkuu wa Mkoa au Askofu, njaa ikiuma linataka kulishwa. Kama kila mtu anahitaji kula, basi ni lazima kila mtu alime. Tutakaowasamehe ni watoto, wazee na wagonjwa,” alisema.

Akifafanua kuhusu wale wenye ulemavu, Waziri Mkuu alisema: “Wako walemavu ambao wanaweza kulima, nao pia walime.”

Alisema yeye ameandaa amri 10 za kuharakisha maendeleo ya mkoa na kuzitaja kuwa ni: Kila mtu lazima ale; kila mtu lazima aondokane na umaskini; kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi ni lazima alime; kila mtu awe na ekari moja ifikapo mwaka 2013 na maandalizi ya shamba yaanze mapema.

“Ekari hizi mojamoja ziwe zinaongezeka kila mwaka ekari moja, yaani mwaka 2014 mtu awe na ekari mbili na mwaka 2015 awe na ekari tatu, mkifanya hivyo mtaona matunda yake,” aliongeza.

Akitaja amri nyingine, Waziri Mkuu alisema kila ekari itakayolimwa ni lazima iwe imepimwa kitaalam kwamba ina ukubwa wa hatua 70 kwa 70; ekari hiyo ilimwe kwa sesa na siyo matuta; ekari hiyo ipandwe kwa kutumia mbegu bora, kwa mistari na kwa nafasi wanazoelekeza wataalamu.

“Ni lazima ekari moja ikupe miche 16,000 ya mahindi. Nalisema hili kwa uchungu kwa sababu nimetembea hapa nchini na nje ya nchi na kuona jinsi wenzetu walivyoendelea kutokana na kilimo,” alisema. “Panda ekari yako kutumia mbole ya minjingu mazao sababu yenyewe haihitaji kuongeza mbolea ya kukuzia na tena panda kwa mstari kwa kutumia kamba,” alisisitiza huku akitumia lugha za Kiswahili, Kifipa na Kipimbwe.

Akitaja amri ya nane, Waziri Mkuu alisema ni lazima palizi ifanyike kwa wakati. Alisema wanapaswa kuvuna kwa wakati na kuhifadhi ghalani mazao yao. “Siku hizi mahindi hayakai ghalani, bali yanaishia kwenye magunia, hii hapana, haifai.”

Akitaja amri ya 10, Waziri Mkuu alizitaka Halmashauri za Mkoa huo, kila kijiji kuhakikisha wanatunga sheria ndogondogo za kuwasaidia wananchi kutekeleza amri hizo.

Aliwataka viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo wawe wakulima kwanza ndipo waisimamie Serikali kuona kama inatekeleza yale iliyoyazimia. Desemba 19, 2012 Waziri Mkuu atakwenda kata ya Majimoto ambako atapokea taarifa ya mnada na kisha atazungumza na wananchi.