Waziri Mkuu Pinda Aahidi Mazao Mbadala ya Biashara

Waziri Mkuu Mizengo Pinda

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewataka wakazi wa wilaya mpya ya Mlele mkoani Katavi walime mazao mbadala ya biashara kama alizeti, karanga na ufuta kwa sababu yanachukua muda mfupi na hivyo kuleta kipato cha haraka.

Ametoa wito huo Desemba 14, 2012, wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nsenkwa mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye zahanati ya kijiji hicho akiwa katika siku ya pili ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.

Waziri Mkuu aliwataka wakazi hao kuachana na mazoea ya kulima tumbaku
kwa vile inachukua muda mrefu hadi kukomaa na inachangia uharibifu
mkubwa wa mazingira kwani inahitaji kuni nyingi wakati wa kukausha.

“Tumbaku hivi sasa haina bei kwa sababu wanaopanga bei ni wakubwa huko
nje…tuangalie mazao ya alizeti, ufuta na karanga kwa sababu yanatoa
pesa kwa haraka zaidi. Mfano mzuri ni Singida ambao wamekuja juu
kiuchumi kwa sababu ya zao la alizeti,” alisisitiza.

Aliwataka wakazi hao waangalie ufugaji nyuki kama fursa ya kipekee kwa
sababu mkoa huo umejaliwa kuwa na misitu mingi na unaweza kuongeza
kipato cha mkoa wao. “Asali ni dawa, asali ni chakula, asali ni
biashara na ina soko hapa nchini hadi nje ya nchi. Changamkieni fursa
hii, ongezeni uzalishaji wa asali na nta,” aliongeza.

Aliwashauri pia waangalie uwezekano wa kulima miembe ya kisasa kwa
sababu inazaa kwa wingi na katika kipindi kifupi mno. “Hii miembe yenu
inazaa maembe 10-20 kwa mwaka lakini ya kisasa inazaa hadi maembe
10,000, ikiwa chinichini tu,” alisema.

Akihimiza kanuni bora za kilimo, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo
la Mlele aliwataka waachane na kilimo cha matuta na badala yake
watumie kilimo cha sesa. “Ekari moja ya mahindi inapaswa ikupatie
magunia 20-25 ya mahindi, sasa wewe unalima ekari tatu na kuvuna
magunia 10, sababu kubwa ni nafasi zinazopotea kwenye miraba ya
matuta, alisema.

“Ni lazima tuondokane na kilimo hiki kwa sababu hakina tija na tena
kinatumia nguvu nyingi na kupoteza eneo kubwa ambalo lingetumika
kupanda mazao,” alisisitiza.

Desemba 16, 2012 Waziri Mkuu atakwenda kata ya Ugalla ambako ataweka jiwe la msingi kwenye mradi wa umwagiliaji maji, atahutubia mkutano wa hadhara na kisha kuelekea Kambuzi Halt ambako atahutubia wananchi.