WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameahidi kutoa trekta moja kwa ajili ya
kikundi cha vijana katika kata ya Ilunde ili waweze kuondokana na
kilimo cha jembe la mkono na waboreshe uchumi wa eneo hilo.
Ametoa ahadi hiyo Desemba 14, 2012, wakati akizungumzana wakazi wa kijiji cha Ilunde kwenye uwanja wa shule ya msingi Ilundekatika siku ya pili ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele,mkoani Katavi.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Katavi alisema atawapatia
trekta hilo kama mkopo ili nao wakirudisha trekta jingine, liweze
kukopeshwa kwa kikundi kingine. “Hapa naanzisha ‘Kopa trekta lipa
trekta’. Litakuja likiwa na jembe lake pamoja na harrow,” alisema
Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
“Ni lazima tuondokane na kilimo cha jembe la mkono kwa sababu hakina
tija… na zaidi nasisistiza kuondokana na kilimo cha matuta kwa
sababu kinatumia nguvu nyingi na kupoteza eneo kubwa ambalo
lingetumika kupanda mazao,” alisisitiza.
Waziri Mkuu alielezwa matatizo yanayowakabili wakazi hao yakiwemo
ubovu wa barabara ya kutoka Inyonga (km. 60) na ukosefu wa wauguzi wa
kike kwa ajili ya akinamama wajawazito. Pia waliomba kupatiwa minara
wa mawasiliano ya simu kwa sababu wanapotaka kupiga simu, wanalazimika
kupanda mti mmoja tu ambao uko km.12 kutoka kijijini hapo.
Akijibu maombi yao, Waziri Mkuu aliwaita Mganga Mkuu wa Wilaya ya
Mpanda na Mhandisi wa Wilaya hiyo ili watoe maelezo kwa wananchi hao.
Kuhusu wauguzi, mganga mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Emmanuel Kamgobe
alisema wanashugulikia suala hilo.
Naye Mhandisi wa wilaya hiyo, Injinia Godfrey Majuto alisema katika
mwaka ujao wa fedha, wilaya imetenga sh. Milioni 60 kwa ajili ya
ukarabati wa barabara ya Inyonga – Ilunde na wameainisha kilometa tano
ambazo ni korofi zaidi.
Mchana huu Waziri Mkuu alifungua bweni la wasichana kwenye shule ya
sekondari ya Ilela ambalo lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 52. Ujenzi
wa bweni hilo umegharimu sh. milioni 36/-.
Naye mbunge wa viti maalum mkoa wa Katavi, Dk. Pudenciana Kikwembe
ameahidi kutoa vyandarua, mashuka na mablanketi kwa ajili ya wanafunzi
wote 52 wa kwanza watakaolala kwenye bweni hilo.
Desemba 15,2012 atakagua kituo cha Afya cha Inyonga
na kuzindua mradi wa madawati kwa shule za Tarafa ya Inyonga.