HALI ya usalama imeimarishwa nchini kote Misri huku Cairo ikijiandaa kwa maandamano mengine yanayowahusisha wafuasi na wapinzani wa katiba mpya iliyopitishwa na serikali ya Misri.
Wanajeshi wanafanya doria kwa kutumia vifaru huku wakiwa wameweka vizuizi vya seng’enge na matofali, nje ya Ikulu ya Rais Mohammed Morsi. Makundi ya upinzani yanataka kura ya maoni ifutwe iliyopangwa kufanyika siku ya Jumamosi juu ya katiba hiyo mpya.
Wafuasi wa bwana Morsi wameitisha maandamano yao kufanyika sambamba na yale ya upinzani.
Rais Morsi anasema kuwa katiba mpya italinda faida zilizotokana na mapinduzi ya kiiraia yaliyomwondoa mamlakani rais Hosni Mubarak mwaka jana, lakini wapinzani wake wanasema anarejesha nchi nyuma, katika mizizi ya kidikteta.
Siku ya Jumatatu, kulikuwa na taarifa za ghasia na vurugu mjini Cairo, huku wapinzani waliokuwa wamekesha katika medani ya Tahrir wakifyatuliwa risasi.
-BBC