WIZARA ya Nishati na Madini imetenga jumla ya sh. bilioni 8.9 kwa dhamira ya kuwainua wachimbaji wadogo wa madini nchini ili kukuza kipato chao na hivyo kuboresha hali zao za kimaisha. Jitihada za kuwainua wachimbaji wadogo zinalenga pia kuinua pato la taifa kutokana na kuongezeka kiwango cha ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali zinazopaswa kulipwa na wachimbaji hao kwa Serikali.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa akizungumza na wajumbe waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wachimbaji wadogo wa madini nchini, uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni.
“Tunayo dhamira ya dhati kuwasaidia ili maisha yenu yaboreke na pia ili kukuza pato la taifa hili”, alisisitiza Waziri Muhongo na kuongeza kuwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ndilo limepewa jukumu la kusimamia mipango ya uendelezaji wachimbaji wadogo kwa kushirikiana na taasisi nyingine mbalimbali zinazohusika na sekta ya madini.
Hata hivyo Profesa Muhongo amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini kuhakikisha wanasajili biashara zao, kuanisha mapato yao, pamoja na kulipa kodi na tozo mbalimbali zinazowahusu ili taifa liweze kunufaika na rasilimali hiyo ya madini. Alisisitiza kuwa wachimbaji watakaofuata vigezo hivyo ndiyo tu watakaopata misaada ya aina mbalimbali ikiwemo mafunzo na mikopo kutoka serikalini na wadau wengine wa maendeleo.
Kwa upande wao, wajumbe waliohudhuria mkutano huo wa siku mbili, ambao ni viongozi na wawakilishi wa vyama vya wachimbaji madini kutoka mikoa yote nchini, waliahidi kuyafanyia kazi maagizo hayo ya Waziri kwa manufaa yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.