Na Mwandishi wa Thehabari, Dodoma
KIKOSI cha Kutuliza Ghasia (FFU) jana mjini hapa kililazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma Kitivo cha Sayansi ya Jamii na Sanaa ya Lugha ambao waligoma na kufanya maandamano kuelekea Bungeni kwa madai ya kukutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Hata hivyo wanafunzi hao hawakufanikiwa baada ya FFU kutanda karibu eneo lote la mji wa Dodoma baada ya kuwatawanya kwa mabomu na kuzuia mkusanyiko wowote wa wanachuo hao.
Mbali na Pinda walipanga pia kumuona Waziri wa Elimu, Shukuru Kawambwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha ili wapewe tamko kutoka kwa viongozi hao kuhusina na fedha za mafunzo kwa vitendo katika Chuo hicho, kwani tayari walipewa ahadi ambayo haijatekelezwa hadi leo.
Maandamano yao yalianza majira ya saa moja asubuhi kutokea chuoni na FFU walianza kupiga mabomu tangu chuoni kwa lengo la kuwatawanya, lakini wanafunzi walitawanyika kila mmoja na kukutana mjini eneo la Viwanja vya Nyerere na kuwasubiri viongozi hao kuja kuzungumza.
Baada ya kukusanyika walianza kuelekea Bungeni bila kujali vitisho vya FFU kwani wapo tayari kufa ilimradi kilio chao kisikike lakini askari wa kutuliza ghasia waliwazunguka katika viwanja hivyo kuwazuia kufika viwanja vya Bunge.
Wanafunzi hao hawakulijali hilo waliendelea na maandamano kuelekea Bungeni na walipofika eneo la shule ya sekondari walikuta askari wametanda kila kona hatimaye askari hao walianza kumwaga mabomu ya machozi mfululizo kwa hilo la kuwatawanya wanafunzi hao washindwe kutimiza azma hiyo.
Kufuatia hali hiyo wanafunzi walianza kuondoka mmoja mmoja wakidhani wangeweza kufika katika viwanja vya Bunge kwa mtindo huo lakini ilishindikana kwani katika eneo hilo na barabara zote zinazolizunguka eneo hilo walikuwa wamewekwa FFU hali iliyowafanya wanafunzi hao kushindwa kufika viwanja vya bunge.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. James Msekela alifika katika eneo hilo lakini aliogopa kuingia ndani ya viwanja hivyo kwani wanafunzi walipomuona tu walianza kumzomea na kudai hawamtaki kwani hawezi kuwasaidia.
Madai ya wanafunzi hao ni kupewa fedha za mafunzo kwa vitendo waliyoanza kuomba tangu mwaka jana na kuonana na Waziri Pinda na viongozi wengine husika kabla ya kuahidiwa wangepewa zoezi ambalo halijatekelezwa hadi leo. Rais wa Kitivo cha Sayansi Asilia, Lema Tumsifu alisema wameshindwa kutumia mazungumzo kwani wameshazungumza vya kutosha lakini hawapati haki zao.
“Hii ni siasa kama wao wanatuletea siasa na sisi tunawaletea siasa, haiwezekani viongozi wanakuja wanatuahidi kututekelezea mahitaji yetu lakini hawatutekelezei,” alisema Lema.
Alisema kuwa wao hawarudi chuoni mpaka viongozi hao wawahakikishie ni lini wataanza mafunzo kwa vitendo kwani haiwezekani mtu wa shahada asome miaka mitatu bila kwenda mafunzo ya vitendo.