Na Anna Nkinda, Maelezo
MKE wa Rais Mama Salma Kikwete ameyataka makampuni na mashirika binafsi kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi ili nao wajisikie kuwa wanahaki ya kupata furaha na mapenzi kama watoto wengine hali hiyo itazididi kuwajengea upendo baina yao na watoto wengine.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ameyasema hayo leo wakati wa chakula cha mchana kwenye sherehe ya mwisho wa mwaka ya watoto yatima iliyofanyika katika viwanja vya Taasisi hiyo vilivyopo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema kuwa alipoanzisha taasisi hiyo moja ya malengo yake ilikuwa ni kuwasaidia watoto yatima na wale wenye uhitaji maalum katika nyanja zote hususani ya elimu.
“Nilipata msukumo wa kufanya shughuli hizi kwani nimeona ni wajibu wangu nikiwa kama mwanamke na vilevile mama wa familia na pia kwa kufahamu kuwa Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa kuboresha elimu kwa jamii hususani watoto hivyo inahitaji kusaidiwa na taasisis zisizo za kiserikali ili kufanikisha suala hili,” alisema Mama Kikwete.
Aliyaomba makampuni hayo wasichoke kuwasaidia watoto hao bali waendelee na moyo wa kuwasaidia kwa kupeleka mahitaji muhimu ya kibinadamu kwenye vituo vyao na kisha kujumuika nao katika hafla kama hiyo kwani ni jambo muhimu sana kwa taifa na kwa watoto kwakuwa wanapata faraja kubwa.
Chakula hicho cha mchana kiliandaliwa na Taasisi ya WAMA kwa kushirikiana na kampuni ya Simenti ya Twiga na Rotary Club. Watoto waliohudhuria sherehe hizo ni kutoka Kituo cha watoto yatima cha Malaika cha Mkuranga, Umra cha Magomeni, Kurasini, Mama Lenga kutoka Kigogo na Kituo cha watoto Yatima cha Kiislamu cha Mwandamila cha Boko.