Ni Uhuru wa Nchi Gani..??

Bendera ya Tanzania

NASIKIA matangazo leo kila mahala kwamba eti kesho kuna maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara.Nimesoma historia,sikumbuki kama katika ramani ya dunia kuliwahi kuwa nan chi iliyoitwa Tanzania Bara na ambayo ilipata Uhuru tarehe 9 Desemba 1961.Kumbukumbu zinanitanabaisha kuwa ilipata kuwapo nchi kwa jina la Tanganyika katika Afrika ya Mashariki na ambayo ilipata Uhuru wake tarehe 9 Desemba 1961.Ni nchi ambayo Babu yangu mzee Emil Lusambo Sr. alipata kuwa raia wake.

Kesho ni miaka 51 tangu ulipozaliwa mama yetu Tanganyika.Hivi kwa nini watoto wako hawapendi kukutaja Eee mama Tanganyika?? Uliwakosea nini watoto hawa mapaka waoni kinyaa kukukumbuka angalau kwa historia tu?? Wala hatutawasahau wazalendo walioyatoa maisha yao kwa ajili yako Tanganyika…oohh,.walotoa jasho lao, waliomwaga damu yao,.waliojitolea kila namna ya tunu walizojaaliwa na mwenyezi Mungu kuhakikisha mama Tanganyika unasitawi, tutawakumbuka.
Waliokatisha mahusiano ya ndoa zao katika kipindi cha ujana wao na kubaki wajane,.Hakika historia ya kweli yako mama Tanganyika itawakumbuka daima.Ingawa sisi tunaokukumbuka tunaonekana wabinafsi na wanaopenda kujitenga,.hatutaacha kukumbuka.

Mimi ninakukumbuka.Mohamed Mikidadi anakukumbuka.George Bosco anakukumbuka.Sophia Shayo anakukumbuka.Athumani Bushiri na wengine wengi wanakukumbuka.Sisi sote tunasikitishwa na upotoshwaji wa Historia unaofanywa na hawa ndugu zetu wa damu.Wanafanya unafiki lakini daima ukweli husimama.

Hakuna taifa linaloweza kuendelea duniani likiwa na msingi katika unafiki.Unafiki ni kielelezo cha woga na kutojiamini.Hatuwezi kujenga amani ya kweli na mshikamano pamoja na maridhiano ya kitaifa juu ya msingi wa Unafiki.Tukijenga juu ya msingi wa unafiki tutavuna woga,kutojiamini na kupungukiwa na uzalendo.Leo hulka ya wanaoitwa waTanzania imekuwa ni woga.Leo dada yangu anatembea barabarani bila kujiamini.Leo kila mtu fisadi kwa kuwa hakuna Uzalendo kwa taifa.
Haya ni matunda machache ya kujenga taifa juu ya msingi wa Unafiki.Muulize Mwanaisha mwanafunzi wa darasa la tatu B shule ya msingi Muungano akuelezee historia ya nchi yake.Utashangaa kusikia mambo ambayo hayaeleweki mwanzo wala wapi yalipo.Historia yetu haieleweki vizuri na wala haifundishwi sawasawa kwa vizazi vyetu.Wenzetu Marekani kwa mfano wana umri wa zaidi ya miaka 200 lakini nchi ni moja yenye mshikamano na amani ya kweli kwa kuwa walijengajuu ya msingi wa ukweli.Kama leo motto wa darasa la tatu hajui historia yake vizuri itakuwaje kwa vitukuu vyetu miaka 250 ijayo?

Tanganyika Heri wanaokutaja na kukumbuka.Heri wanaokulilia leo. Kwa kuwa ukweli hushinda naamini si muda mrefu utaturudia mama yetu.Tunajivunia wewe kuwa mama yetu.Tunajivunia utajiri wa rasilimali ulizanazo ambazo sisi ni waeithi ee mama yetu.Wanaoona aibu kukutaja wasamehe mama,.ila sisi tutakutaja kwa gharama yoyote.Mungu akujalia uzima na afya tele katika kipindi hiki kigumu. Ni mapito tu,tunajua kama sio kesho basi keshokutwa utaturudia tena na tutaishi pamoja nawe mama yetu.Tunakupenda mama yetu.NI UHURU WA NCHI GANI??

CHANZO: Wanabidii (elusambo@gmail.com)