Na Thomas Dominick, Mara
JESHI la Polisi mkoani Mara limekanusha uvumi wa kutishia raia unaotolewa na baadhi ya wananchi wenye nia mbaya kwa vyombo vya habari nchini kuwa ndani ya mwezi mmoja takriban watu 15 wameuwawa kwa kuchinjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalumu ofisini kwake jana, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa huo, Japhet Lusingu alisema kuwa kumekua na uvumi kuwa katika Mkoa huo wananchi wamekuwa wakichinjwa na tayari watu 15 wameuwawa kwa kuchinjwa kitu ambacho amedai ni uzushi.
Kamanda Lusingu alisema kutokana na uvumi huo wamekua wakipokea simu toka kwa wananchi na viongozi ndani ya Manispaa ya Musoma katika Kata ya Nyakato kwamba kuna mwanafunzi ameonekana ameuwawa kwa kukatwa kichwa katika makaburi ya Musoma Bus na Jeshi la Polisi likifuatilia wanakuta ni taarifa za uongo na za kuwatisha wananchi.
Alisema kuwa matukio mawili ndiyo yaliyoripotiwa ambapo wanawake wawili waliuawa kati yao ni Blandina Peru (28) mkazi wa Kijiji cha Mahare, Kata ya Etaro ambapo aliuwawa Desemba 2 mwaka huu kwa kukatwa koromeo na kubakwa na wauaji kabla ya kumuua wakati akiwa porini akikata kuni na watuhumiwa wa tukio hilo bado hawajakamatwa.
Tukio la pili lilitokea Kabegi kata ya Nyakatende wilayani butiama ambapo Sabina Mkireri (44) mkazi wa Kijiji cha Kiemba aliuawa kwa kuchinjwa shingoni na kichwa chake kuchukuliwa na watu wasiojulikana katika Kijiji cha Kabegi na watu sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano.
Kutokana na uvumi huo kiongozi huyo amewatoa hofu wananchi juu ya mauaji hayo na kuwatahadharisha akina mama hasa maeneo ya vijijini wanapokua katika shughuli zao za kilimo na utafutaji wa kuni wawe waangalifu na watoe taarifa mapema wanaposhuku jambo lolote lisilo lakawaida.
“Nachukua nafasi hii kuwatoa hofu wananchi juu ya uvumi uliozagaa wa mauaji hayo na nawatahadharisha akina mama hasa maeneo ya vijijini wanapokua katika shughuli zao za kilimo na utafutaji wa kuni wawe waangalifu na watoe taarifa mapema wanaposhuku jambo lolote lisilo la kawaida,” alisema Lusingu.
Kwa upande mwingine Jeshi hilo limewaomba waandishi wa habari kupata taarifa kutoka kwenye vyanzo husika pia kwa watu ambao wanaoanzisha uvumi wakibainika wanatoa habari za uvumi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Aliongeza kuwa kwa sasa wanaendelea na msako maeneo mbalimbali ya manispaa ya Musoma na wilaya ya butiama ambapo kuna watu watano wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kwa makosa yakupatikana na pombe haramu ya gongo na wengine wanashikiliwa kwa kupatikana na bangi na wote watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Chanzo: www.habarimotomotomara.blogspot.com