Kozi ya Leseni ‘C’ Kufanyika Arusha Desemba 10

Tanzania Football Federation Logo

Na Mwandishi Wetu

KITUO cha Kukuza Vipaji cha Rolling Stone kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kimeandaa kozi ya leseni C ya walimu wa mpira wa miguu itakayofanyika kuanzia Desemba 10, 2012 hadi Desemba 23, 2012 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha. Kozi hiyo itahusisha makocha walio na Cheti cha Kumaliza Elimu ya Sekondari au wale waliohitimu kozi ya ualimu wa mpira wa miguu ya ngazi ya kati (intermediate).

Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni alisema kuwa washiriki wa kozi hiyo wanatakiwa kuwa wamewasili Arusha ifikapo Desemba 9, 2012 na wanatakiwa kwenda na vyeti vyao halisi vya elimu. Alisema tayari Rolling Stone wameshasajili walimu 25 ambao watashiriki kozi hiyo na hivyo kuwataka watu wengine wanye sifa kutoka mkoa wa Arusha na mikoa mingine kujitokeza kushiriki mafunzo hayo muhimu.

Kayuni alisema kuwa kadri taifa litakavyozalisha walimu wengi, ndivyo taifa litakavyokuwa na uwezo wa kuandaa watoto na vijana wengi katika misingi sahihi ya mpira wa miguu na hivyo kuwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri. Kozi hiyo itaendeshwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Kayuni kwa kushirikiana na mkufunzi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF), Bw. Dominic Niyonzima kutoka Rwanda.
Kwa mujibu wa Rolling Stone, kila mshiriki atajigharimia nauli ya kwenda Arusha na atatakiwa kwenda na ada ya fedha zinazolingana na Dola 100 za Kimarekani (dola moja ni sawa na Sh1,580 za Tanzania).

Sita wapitishwa kuwania uongozi TAFCA Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Waliku wa Mpira wa Miguu (TAFCA) imetangaza matokeo ya usaili wa wagombea uongozi chama hicho, ikiwa imepitisha wagombea sita sita na kuwaengua wagombea watano kwenye nafasi tofauti. Baada ya usaili wa wagombea hao, Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA iliwaengua wagombea hao watano kwa kutokidhimasharti ya Ibara ya 26 (2) ya Katiba ya TAFCA na Kanuni ya 9 ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF na pia kutokidhi utashi wa masharti ya 11 (1) ya kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Katika nafasi ya mwenyekiti Oscar Don Korosso alipitishwa kuwa mgombea pekee baada ya Kenedy Mwaisabula na Jamhuri Kihwel kuenguliwa kwa kutokidhi masharti ya ibara ya 26 (2) ya Katiba ya TAFCA na kanuni ya tisa ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF. Katika nafasi ya makamu mwenhyekiti, Kamati imempitisha Lister J. Manyara kuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo huku Marco Bundara akipitishwa kuwa mgombea pekee wa nafasi ya katibu mkuu wa TAFCA.

Hali kadhalika wagombea wawili wa nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu wa TFF, Wilfred Kidau na Magoma Rugora wamekidhi masharti ya Katiba ya TAFCA na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF na hivyo watachuana kuwania kura za wajumbe wa mkutano mkuu, huku Ally A Mtumwa akienguliwa kwa kutokidhi masharti ya kanuni ya 11 (1) ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Katika nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji, wagombea wote wawili, Abubakar Balingula na Aboubakar Salum wameenguliwa kwa kutokidhi masharti ya Ibara ya 26 (2) ya Katiba ya TAFCA na Kanuni ya 9 ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.