POLISI sita na raia 138 wameuawa kwenye matukio ya ujambazi wa kutumia silaha, kati ya Januari na Septemba mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imetoa siku 30 kuanzia leo kwa watu wote wanaomiliki silaha kinyume cha utaratibu kuzisalimisha kwa hiari yao, ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi.
Dk Nchimbi alisema hatua hiyo inatokana na kuongezeka kwa matukio ya uhalifu wa kutumia silaha, kwani tangu Januari hadi Septemba mwaka huu kumebainika kuwapo kwa matukio 876.
“Matukio hayo yamesababisha vifo vya raia 138 na polisi sita, mali zenye thamani ya Sh4,560,389,970 ziliibwa kwa kutumia silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria, zikiwamo nyingine zinazomilikiwa kisheria lakini zinatumika isivyo halali,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:
“Kufuatia hali hiyo natoa wito kwa mtu yeyote au kikundi chochote kinachomiliki silaha kinyume cha sheria kuisalimisha vituo vya polisi, kwa wenyeviti wa vitongoji/vijiji, watendaji wa kata, taasisi za dini, wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa.”
Alisema atakayesalimisha silaha kwa hiyari ndani ya kipindi hicho hatachukuliwa hatua zozote za kisheria.
“Kwakweli baada ya muda huo kumalizika yaani Januari 5, mwakani operesheni kali itafanyika nchi nzima na yeyote atakayebainika akimiliki silaha isivyo halali na kinyume cha sheria atakamatwa na sheria itachukua mkondo wake,” alisema Waziri Nchimbi.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz