Na James Gashumba, EANA-Arusha
MKUTANO wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliomalizika mwishoni mwa wiki, umeahirisha kufanya uamuzi juu ya maombi ya nchi za Sudan Kusini na Somalia kujiunga na jumuiya hiyo ya kiuchumi yenye wanachama watano.
Sudan Kusini ilioomba kujiunga na EAC miezi michache tu baada ya kupata uhuru wake mwaka jana wakati Somalia iliwasilisha maombi yake Februari, 2012, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) linaripoti. Aprili, mwaka huu, viogozi wa kanda hiyo walipokutana mjini Bujumbura, Burundi, waliahirisha kufanyia maamuzi maombi ya Sudani Kusini, hadi Novemba.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa mwishoni mwa mkutano huo, imeuelekeza Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa EAC, ambao ni chombo cha kufanya maamuzi cha jumuiya hiyo, kufanya majadiliano zaidi na nchi hiyo mpya kabisa duniani na kuzingatia pia ripoti ya kamati ya tathmini juu ya suala hilo.
Maamuzi hayo yalifikiwa baada ya viongozi hao wa nchi wanachama; Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi kupokea taarifa ya maendelea ya maombi ya Sudani Kusini, kujiunga na EAC. Sababu za kuahirishwa kukubaliwa kwa maombi ya nchi hizo mbili hazijafahamika.
Lakini kikao cha mwisho kilichofanyika mjini Nairobi, Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Kenya, Musa Sirma alisema matukio ya mgogoro kati ya Sudani Kusini na jirani yake Sudani unaweza kuathiri nia ya nchi hiyo ya kutaka kujiunga na EAC.
Kuhusu ombi la Somalia, mkutano wa wakuu wa EAC pia umeuelekeza Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa EAC kuanza mchakato wa uhakiki wa maombi hayo na kuwasilisha taarifa katika mkutano wa 15 wa wakuu hao.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wake mpya, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, alisisitiza umuhimu wa kutumia rasilimali zote zilizozopo kuimarsiaha mtangamano.
“Kadiri tunavyoendelea na mchakato wa mtangamano, tunahitaji kufanya tathmini ya vigezo tulivyonavyo; eneo la ardhi, madini, maji na rasilimali watu. Vyote kwa pamoja ni muhimu katika mtangamano wetu na hatuna budi kuvithamini,” Rais Museveni alisema.