Mgawo wa umeme wairudisha TANESCO katika kero kwa wateja

Mitambo na mafundi wa TANESCO

Na Waandishi Wetu, hudumabongo@gmail.com

UCHUNGUZI uliofanywa na wanahabari katika zoezi la kukusanya kero za sekta binafsi linaondelea kupitia mitandao ya jamii ya Twitter na Facebook umeonyesha kuwa wakazi wa jijini Dar es Salaam wanakabiliwa na mgao wa umeme kwa kipindi kirefu sasa.

Hali hiyo imebainika wakati wa majumuisho ya kero za wateja wa huduma na bidhaa mbalimbali nchini Tanzania katika mzunguko wa tatu ambapo Shirika la Ugavi wa Umeme TANESCO limechukua nafasi ya kwanza kati ya biashara 36 zilizotajwa kuwa kero kwa wateja.

Jumla ya kero tofauti 220 zimewasilishwa na wateja toka zoezi hilo lianze ambapo Shirika la Tanesco lina jumla ya kero 71 ambapo kati ya hizo 60 ni kutoka Dar es Salaam pekee.

Katika mzunguko huu nafasi ya pili ilishikiliwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo yenye kero 63 kati ya 220 huku nafasi ya tatu ikiwaendea Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom yenye kura 17 kati ya 220 zilizowasilishwa.

Hakukuwa na mabadiliko makubwa katika makundi mengine ambapo washindi wa kero ni wafuatao Precision Air (Huduma za Anga) CRDB (Huduma za Kibenki) StarTimes (Ving’amuzi) DAWASCO (Huduma za Maji Safi na Taka mkoani DSM) SHOPRITE- (Wauzaji wa bidhaa mbalimbali)

Katika mzunguko huu jumla ya biashara 4 zimeingia katika mchuano huo nazo ni Mara Milk, Zanzibar Insurance, Bonjour Petrol Station na Coca Cola (Nyanza Bottlers)

Kwa maelezo zaidi juu ya utaratibu wa kura na zoezi hili linavyofanyika tembelea link ifuatayo http://bit.ly/10SARH1

Huduma Bongo inatoa wito kwa vyombo vya habari nchini kufuatilia kwa makini kero hii ya mgao wa umeme unaofanyika kwa siri na utaalamu wa hali ya juu na kuleta usumbufu mkubwa kwa wanajamii na hasara kwa wafanyabiashara.