WANADAI kutengwa kwa rasilimali za kutosha kupambana na Ukatili wa Kijinsia
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na mitandao ya kutetea haki za binadamu, ukombozi wa wanawake Kimapinduzi na masuala ya Jinsia pamoja na wanaharakati wa Semina za Jinsia na Maendeleo ( GDSS), leo tunaungana na Jumuiya ya Kimataifa na wanaharakati wenzetu nchini kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Tanzania, Afrika na duniani kote.
Lengo la maadhimisho haya ni kutoa fursa kwa wanawake na wanaharakati wengine kukuza uelewa wa umma juu ya mchango wa wanawake katika maendeleo na kutafakari matokeo ya harakati za wanawake katika kupinga ukatili wa kijinsia Tanzania.
Tunaandhimisha siku hii ikiwa na kauli mbiu ya: Funguka. Kemea Ukatili dhidi ya wanawake. Sote tuwajibike. Wakati sisi TGNP tukiwa na kauli mbiu inayosema: Tokomeza Ukatili wa Kijinsia: Jitokeze kutoa maoni katika katiba mpya.
TGNP na wanaharakati wengine duniani tuaandhimisha siku ya leo kupinga mifumo na tamaduni ambazo zimejikita kwenye jamii ambazo ni za kinyonyaji na kiunyanyasaji zinazowanyima wanawake fursa za kufanya shughuli za kimaendeleo.
Tumeshuhudia ongezeko kubwa la ukosefu wa ajira hasa kwa wanawake na wasichana, uporaji wa rasilimali za taifa – ardhi, misitu madini nk, kukithiri kwa girls trafficking (biashara haramu ya kuuza wasichana nje na ndani ya nchi), ukosefu wa maji safi na salama, ukosefu wa hudumu za afya ya uzazi nk.
Tunaendelea na harakati zetu kupinga kwa nguvu zote matukio yote ya ukatili wa kijinsia kama vile ubakaji nje na ndani ya ndoa, wanawake kunyimwa mirathi wanapofiwa na waume zao, mimba za utotoni, kuozwa kwa nguvu, wanawake kufanya kazi nyingi na kwa muda mrefu zisizokuwa na malipo kama vile kulea watoto, kuhudumia wagonjwa wa UKIMWI /VVU, kupika, kusaka maji umbali mrefu nk . Takwimu zinatuambia asilimia 56% ya wanawake walishawahi kufanyiwa ukatili wa kijinisa, wakati huo huo, asilimia 66% ya wanawake wanafanya kazi zisizokuwa na malipo, asilimia 39.5% ya wanawake hawajasoma ukilinganisha na asilimia 25.3% ya wanaume. Na inasikitisha zaidi kuona kuwa wanawake ni asilimia 80% ya nguvu kazi vijijini na asilimia 60% ndio wazalishaji wakuu wa chakula. Huu ni ukatili wa Kijinsia na ni kinyume na mikataba yote Tanzania iliyoridhia kuhusu haki za wanawake na walemavu (CEDAW, CRC, ILO Convention)
Tumeshuhudia wasichana walio wengi wakikosa elimu bora hasa kutokana na mila potofu zilizopitwa na wakati, wasichana kubebeshwa majukumu mazito ya kuhudumia familia wakati watoto wa kiume wanapewa fursa na muda mrefu wa kujisomea.
Ili kuondoa kabisa ukatili wa Kijinsia Wanawake tunadai yafuatayo yaingizwe Katika katiba mpya:
1. Kutengwa kwa bajeti zenye mtizamo wa kijinsia na kuboresha sera, sheria na mipango husika ili iweze kunufaisha wanawake, wamaume hasa walioko pembezoni. Rasilimali zielekezwe zaidi kwenye madawati ya Jinsia yaliyoko katika vituo vya Polisi, ili kuwezesha ufanisi mzuri wa kazi.
2. Katiba ibatilishe sheria zote zinazokinzana na haki za msingi za wanawake na watoto wa kike hususani kubatilisha sheria na mila zote za ubaguzi wa jinsia katika masuala ya ndoa, mirathi, haki za kumiliki. Kwa mantiki hii, Katiba ibainishe kwa uwazi wajibu wa serikali wa kuchukua hatua zote za kisera na sheria ili kulinda na kuhifadhi haki za wanawake katika maeneo hayo.
3. Katiba iwajibishe serikali kutekeleza mikataba yote iliyoridhia kuhusu haki za wanawake na walemavu (CEDAW, CRC, ILO Convention). Mikataba hii itambulike kuwa ni sheria za nchi ili kuepusha ucheleweshaji.
4. Katiba iweke misingi ya kulinda utu wa mwanamke dhidi ya uonevu na ukatili wa jinsia ndani ya ndoa na kwenye jamii, ikiwa ni pamoja na kukataza ubakaji ndani ya ndoa, kukataza mila zinazomdhalilisha mwanamke, (tohara, kurithiwa bila hiari) na kubainisha haki sawa ndani ya ndoa, kukataza ndoa za utotoni za watoto wa kike. Serikali iwajibishwe kuchukua hatua za kisera na kisheria kuimarisha utekelezaji wa haki hizi.
Katiba iweke wazi kuwa rasilimali za taifa lazima ziwanufaishe wananchi wote na mapato/ fedha zilizotokana na uchumi wa nchi ziwekwe kwenye benki za hapa hapa nchini mfano mapato yatokanayo na mafuta, gasi asilia, madini, mbuga za wanyama na utalii